Watanzania watamba Rock City Marathon

Watu wenye ulemavu wa ngozi wakiwa katika mashindano ya mbio za Rock City Marathon kwa umbali wa kilometa tano jijini Mwanza, jana. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Mwanariadha Chacha Boi aliibuka mshindi kwa wanaume na kujinyakulia Sh1.5 milioni, medali na cheti.

Mwanza. Watanzania wameng’ara kwenye mbio za Rock City Marathon 2016 zilizofanyika jana na kujinyakulia zawadi mbalimbali.

Mwanariadha Chacha Boi aliibuka mshindi kwa wanaume na kujinyakulia Sh1.5 milioni, medali na cheti.

Boi aliibuka mshindi wa kilomita 21 kwa kutumia saa 1:03:00 na kumbwaga mpinzani wake, David Kilimo kutoka Kenya aliyeibuka mshindi wa pili kwa kutumia saa 1:04:40 na kujinyakulia Sh900,000, medali na cheti na Moris Mosima aliyetumia saa 1:40:33 na kuzawadiwa Sh 700,000, medali na cheti.

Wanawake kwenye kilomita 21, Faimina Abdi kutoka Arusha aliibuka mshindi kwa kutumia saa 1:13:12 na kujinyakulia Sh 1.5 milioni, medani na cheti, akifuatiwa na Angelina Daniel pia kutoka Arusha aliyekabidhiwa Sh 900,000, medali na cheti na nafasi ya tatu ikienda kwa Derofina Omary, raia wa Kenya aliyepewa Sh700,000, medali na cheti.

Walemavu wanaume waliokuwa wakikimbia kilomita tano, Bernard Samike aliibuka mshindi na kupewa Sh 50,000, Mishuda Mayenga 40,000 na Kusekwa John, Sh 30,000.

Wanawake, mshindi alikuwa Helena Bahati aliyepata Sh50,000, Helena Ngillo Sh40,000 na Leticea Michael, Sh30,000.

Mbio za kilomita tatu zilizohusisha wazee kwa upande wa wanaume, Jeremia Kinshuri aliibuka mshindi na kujipatia Sh50,000, Muzungu Makaranga Sh30,000 na Deus Majige Sh20,000.

Wanawake mshindi alikuwa Christina Felix aliyezawadiwa Sh50,000, Sauda Chiza na Tatu Buta kila mmoja Sh20,000.

Ni mara ya pili kwa Tanzania kuibuka washindi kwenye mbio hizo za msimu wa nane. Mwaka 2013 Mwita Kopiro aliibuka mshindi.

Meneja wa benki ya Posta tawi la Mwanza, Shaaban Telatela alisema waliamua kushiriki mbio hizo kwa lengo la kutangaza utalii ili kuinua uchumi.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi, Zenno Ngowi alisema watahakikisha mbio hizo msimu ujao wanaziboresha na kwamba tayari wameanza mazungumzo na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) ili ziwe za kimataifa na kuwekwa kwenye kalenda yao.