Yanga yaifuata Kagera kwa tahadhari

Muktasari:

Ni mahali ambako imekumbana na upinzani mkali

Mwanza. Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema anakwenda Bukoba mkoani Kagera kwa tahadhari kubwa kuwavaa Kagera Sugar Jumamosi baada ya kupata habari zao kuwa wanapokuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba wanakuwa wagumu kufungika.

Yanga haina matokeo mazuri kwenye uwanja huo uliopo mjini Bukoba na itawavaa Kagera Sugar, mahali ambako mara ya mwisho ilitunguliwa bao 1-0.

Wakati kocha huyo akitamka hayo, nyota wa timu hiyo, Haruna Niyonzima na Simon Msuva wamesema Ligi Kuu msimu huu imekuwa ngumu, hivyo kila mchezo watakaocheza utakuwa kama fainali kwao ili kujiweka vizuri kutetea ubingwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, kocha Pluijm ambaye hajawahi kucheza na Kagera kwenye uwanja wake wa Kaitaba alisema anajua ugumu wa timu hiyo inapokuwa nyumbani, hivyo anakwenda kupambana kupata pointi tatu.

Alisema Kagera si timu ndogo, hivyo hawezi kuwadharau na kuongeza kuwa mipango yake ni kuondoka na pointi sita Kanda ya Ziwa ambazo alishanyakua tatu dhidi ya Toto Africans.

“Kagera Sugar ni timu imara, huwezi kuwadharau na pia nasikia ni wazuri wanapokuwa kwenye uwanja wao wa Kaitaba, hivyo nasi tumejipanga kupambana nao,” alisema.

Hata hivyo, winga Msuva alisema wao hawana wasiwasi katika kutetea ubingwa msimu huu licha ya ligi kuwa ngumu.

Msuva alisema kwa sasa malengo yao wachezaji ni kushinda kila mchezo na hilo linawezekana.

Alisema kila mchezo kwao ni fainali na kwamba, hawaangalii mpinzani wao Simba yukoje, isipokuwa wanachopigania ni kuhakikisha wanakusanya alama tatu kila mchezo. “Ligi ni ngumu, lakini sisi hatuangalii cha Simba wakoje, isipokuwa tunachokipigania ni pointi tatu ili kuhakikisha tunachukua tena ubingwa,” alisema Msuva.

Niyonzima alisema timu yao imeimarika na kwamba, kupoteza mchezo hakujaathiri chochote.

“Yanga ni timu nzuri, kila mmoja anaijua, nimerejea baada ya kukaa nje kwa mechi mbili kutokana na hali ya kiafya, ila nitahakikisha ninafanya kile mashabiki wanakihitaji kwangu,” alisema Niyonzima anayevaa jezi namba nane.