Yanga yamkana Lwandamina

Kocha George Lwandamina alipotua jijini Dar es Salaam jana Jumapili.

Muktasari:

George Lwandamina Kocha aliyeiwezesha Zesco kufika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa Afrika alitua nchini huku taarifa zikieleza kuwa amekuja kumalizana na uongozi wa Yanga.

Dar es salaam. Klabu ya Yanga imesema haijafanya mazungumzo yoyote na George Lwandamina ili kuwa Kocha mkuu wa timu hiyo na kusisitiza bado Hans Pluijm ataendelea kuwa Kocha wa timu hiyo.

George Lwandamina Kocha aliyeiwezesha Zesco kufika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa Afrika alitua nchini huku taarifa zikieleza kuwa amekuja kumalizana na uongozi wa Yanga.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ameliambia gazeti hili  leo kuwa uongozi wa Yanga hauna taarifa juu ya ujio wa Lwandamina na wala haujafanya mawasiliano yoyote naye.

"Kwanza hizo taarifa ndio nazisikia kwako.Hatujazungumza naye na wala hatujui kama amekuja,anaweza akawa amekuja kwa shughuli zake.Kocha wa Yanga ni Pluijm (Hans)," amesema Deusdedit

Tangu wiki iliyopita kumekuwa na  taarifa kuwa Yanga inajiandaa kufanya mabadiliko katika benchi la ufundi kwa  kumwondoa Pluijm.