Yanga yanasa mtego wa Simba

Mshambuliaji wa Kagera Sugar,Danny Mrwanda(kushoto) akiwania mpira na beki wa African Lyon,Isihaka Hassan wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika uwanja wa Taifa,Dar es Salaam jana. Kagera ilishinda 2-0.Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Yanga imeingia katika mtego huo baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stand United mjini Shinyanga, ikiwa ni wiki moja kabla ya kukutana na Simba.

Dar es Salaam. Majimaji ya Songea mkoani Ruvuma imeweka rekodi ya kipekee baada ya kufungwa mabao 11-0 katika mechi tatu ilizocheza jijini Dar es Salaam dhidi ya Simba, Yanga na Azam, lakini hilo si jambo kubwa zaidi ya lile la Yanga kunasa kwenye mtego wa watani wao, Simba.

Yanga imeingia katika mtego huo baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stand United mjini Shinyanga, ikiwa ni wiki moja kabla ya kukutana na Simba.

Februari mwaka jana, Simba ilipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United wiki moja kabla ya kuivaa Yanga, Machi 4 mwaka huo. Walipokutana na watani zao, Yanga walifungwa bao 1-0.

Stand United iliyokuwa ikicheza soka la kubutuabutua bila ufundi wowote ilipata bao kupitia kwa Pastory Athanas, ambaye aliwazidi akili mabeki wa Yanga, Andrey Vincent na Mwinyi Haji.

Kipigo hicho kilikuwa cha kwanza kwa Yanga kwenye mechi za Ligi Kuu tangu ilipofungwa na Coastal Union kwa mabao 2-0 Januari mwaka huu, ikiwa imekaa miezi saba na siku 27 bila kufungwa.

Wakati Yanga ikipokea kipigo hicho, imeshuhudia pia washambuliaji wake wawili,

Amissi Tambwe na Donald Ngoma wakiwa na wastani mbovu wa mabao kwa dakika, Ngoma amefunga bao moja katika dakika zaidi ya 432 alizocheza msimu huu, huku Tambwe akiwa amefunga mabao matatu katika dakika 450.

Wakati ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji ukiiendelea kuiimarisha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 16, baada ya kuibuka na ushindi kwenye mechi tano na kutoka sare mara moja.

Furaha hiyo ya Simba haikuishia kwenye kuongoza ligi tu bali pia mshambuliaji wao, Shiza Kichuya alipachika mabao mawili yaliyomfanya aongoze kwenye chati ya ufungaji mabao akiwa ameziona nyavu mara nne.

Safu ya ushambuliaji ya Simba imeonyesha haimtegemei mtu mmoja msimu huu kwani pamoja na mshambuliaji wao wa kati akiwamo Laudit Mavugo, ambaye hakuwa katika kiwango bora, timu hiyo ilipata mabao manne kupitia kwa washambuliaji wake wa pembeni, Kichuya na Jamal Mnyate, ambao kila mmoja alifunga mawili.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema msimu huu timu yao imeimarika kila idara na haimtegemei mtu mmoja kupata matokeo na ndiyo sababu ilipata ushindi wa kishindo.

Katika mchezo dhidi ya Majimaji, mshambuliaji Frederick Blagnon, raia wa Ivory Coast hakujumuishwa katika kikosi wakati Ibrahim Ajibu akiumia dakika ya 23 na kulazimika kutolewa.

“Ni kweli Mavugo (Laudit) hayupo katika kiwango bora, lakini hiyo si sababu ya sisi kushindwa kufanya vizuri, timu yetu kwa sasa ina watu wengi wenye uwezo wa kufunga, wakishindwa washambuliaji wa kati hata wa pembeni watafunga,” alisema Mayanja.

Katika mchezo dhidi ya Majimaji, kocha Joseph Omog alijaribu kumwanzisha beki Mganda, Juuko Murshid sambamba na Mzimbabwe, Method Mwanjali kwa mara ya kwanza ikiwa ni ishara kuwa pengine kocha huyo amesikia kilio cha wapenzi wa klabu hiyo, ambao wanaamini kuwa Juuko bado ana nafasi katika kikosi cha kwanza cha kocha huyo, raia wa Cameroon.

“Tuna mabeki bora watatu wa kati kwa sasa, anapocheza yeyote tunakuwa na amani, hii ndiyo sababu alicheza Juuko na Mwanjali katika mchezo na Majimaji,” alisema Mayanja.

Murshid alisema kwa sasa wanahamishia nguvu katika mchezo dhidi ya Yanga.

“Mechi zilizopita zimepita. Wote kwa sasa tunaifikiria Yanga. Ni mechi ngumu lakini tunajiandaa na kuupa umuhimu mchezo huo kama iliyopita,” alisema beki huyo.

Azam imepotea wapi

Kuondoka kwa washambuliaji wanne wa Azam, Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu na Allan Wanga na Ame Ali aliyetolewa kwa mkopo kumeendelea kuigharimu timu hiyo, ambayo ilipoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kufungwa na Ndanda ya Mtwara kwa mabao 2-1.

Awali Azam ilifungwa bao 1-0 na Simba kabla ya kusafiri kwenda Mtwara.

Bao la John Bocco halikutosha kuwafanya Azam wanusurike mbele ya Ndanda inayoonekana kuwa tishio nyumbani, ambayo ilipata mabao yake kupitia kwa Riffat Khamis na Hajji Mponda.

Mbali na kubomoka kwa safu hiyo ya ushambuliaji, Azam bado inapata wakati mgumu katika safu yake ya ulinzi kutokana mabeki wake wawili wa kutumainiwa, Sergie Wawa na Aggrey Morris kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu sasa.

Maafande wa JKT Ruvu waliamka kutoka usingizini na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, wakati mkosi ukiendelea kuiandama Mwadui FC inayonolewa na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons.

Sare hiyo imeifanya Mwadui FC kucheza dakika 450 za Ligi Kuu bila kupata ushindi na kuwashusha hadi nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

Mbao FC nayo ni kama imefufuka upya kwani ilifanikiwa kulazimisha sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar ugenini. Timu hiyo imefanikiwa kuvuna pointi nne kati ya tisa kwenye mechi zake tatu za ugenini dhidi ya Ruvu Shooting, African Lyon na Mtibwa.