Yanga yaruhusiwa kutumia U/Taifa

Muktasari:

Katika mkataba huo, Yanga imeruhusiwa kutumia viwanja hivyo kama viwanja vyake vya nyumbani kwa sharti la kuvitunza.

Dar es Salaam. Serikali imesaini mkataba na Klabu ya Yanga kutumia Uwanja wa Taifa na wa Uhuru kwa ajili ya michezo yote ya kimataifa na ya Ligi Kuu ya ndani.

Mkataba huo umesainiwa jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel kwa niaba ya Serikali na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit kwa niaba ya klabu yao.

Katika mkataba huo, Yanga imeruhusiwa kutumia viwanja hivyo kama viwanja vyake vya nyumbani kwa sharti la kuvitunza.

Miongoni mwa masharti hayo ni kutunza viwanja, mali na vifaa vyote vilivyopo katika viwanja hivyo, na endapo kutatokea uharibifu wowote utakaofanywa na wachezaji ama mashabiki, klabu hiyo itawajibika kubeba gharama za matengenezo yote.

Aidha, Yanga inaweza kutumia viwanja hivyo kwa mazoezi ya kujiandaa na mechi zinazowakabili.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Yanga, Deusdedit alisema ni kweli sheria ya klabu ya leseni imewalazimu kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na uwanja, hivyo imebidi wasaini mkataba wa makubaliano na Serikali.

Yanga ilizuiwa kutumia Uwanja wa Taifa pamoja na Simba baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika Oktoba Mosi kutokana na mashabiki wanaosadikiwa kuwa wa Simba kung’oa viti.