Zimbabwe kuibeba Senegal leo

Muktasari:

Senegal itashuka katika mchezo huo ikiwa na pointi tatu, wakati Algeria na Zimbabwe zikiwa na pointi moja moja huku Tunisia ikiwa mikono mitupu.

Franceville, Gabon. Senegal inaweza kuwa timu ya kwanza kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Mataifa ya Afrika kama itaibuka na ushindi dhidi ya Zimbabwe mjini Franceville leo.

Senegal itashuka katika mchezo huo ikiwa na pointi tatu, wakati Algeria na Zimbabwe zikiwa na pointi moja moja huku Tunisia ikiwa mikono mitupu.

Majirani hao wa kaskazini mwa Afrika wanakutana katika mchezo wa kwanza nchini Gabon.

Kufuzu kwa hatua hiyo huku ukiwa na mchezo mmoja mkononi kunaweza kuleta mabadiliko kwa Simba wa Teranga baada ya kushindwa kufanya hivyo katika fainali mbili za Mataifa ya Afrika.

Ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo zinapewa nafasi ya ubingwa wakati Gabon walipokuwa wenyeji wa fainali hizo 2012, Senegal ilichapwa na Zambia, pamoja na Guinea ya Ikweta na kucheza na Libya ikitoka mapema zaidi.

Miaka mitatu baadaye walirudi Guinea ya Ikweta baada ya kuifunga Ghana, kwenda sare na Afrika Kusini na kufungwa na Algeria na kutolewa tena katika mzunguko wa kwanza.

Kocha na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Aliou Cisse anaona kuwa Senegal haiwezi kufanya makosa yaliyopita msimu huu.

“Labda tulijihamini kupita kiasi katika masindano yaliyopita kwa vyombo vya habari kutupa nafasi ya ubingwa,” Cisse aliwaambia waandishi wa habari juzi.

“Naamini kwa sasa kuna morali ya juu kikosini, tunajiamini kuwa ni miongoni mwa timu zinazosaka ubingwa huu wa Afrika kwa mara nyingine.

“Tuna kikosi kizuri cha kufika mbali na kutwaa ubingwa kupeleka taji Senegal kwa mara ya kwanza, lakini tuna mechi nyingi ngumu mbele yetu.

“Muhimu ni kuongeza umakini kwa kila mchezo ambao tunashuka uwanjani, naamini tuna uwezo mzuri msimu huu,” alisema.