Zulu asaini Yanga, Mghana kamili...

Kiungo mpya wa Yanga, Justin Zulu akisaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo jana.

Muktasari:

Jana, kiungo Justine Zulu, raia wa Zambia alisaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga, huku klabu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani ikianza harakati za kumnasa mshambuliaji mahiri wa AC Leopards ya Congo Brazzaville, Winston Kalengo.

Dar es Salaam. Usajili wa dirisha dogo umeshika kasi ya aina yake baada ya watani, Yanga, Simba kunasa saini za wachezaji wa kigeni kutoka Zambia na Ghana.

Jana, kiungo Justine Zulu, raia wa Zambia alisaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga, huku klabu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani ikianza harakati za kumnasa mshambuliaji mahiri wa AC Leopards ya Congo Brazzaville, Winston Kalengo.

Watani zao Simba, jana walimpa mkataba wa mwaka mmoja kipa wa Medeama ya Ghana, Daniel Agyei.

Zulu aliyetokea Zesco United alisaini mkataba wake jana mchana kwa dau ambalo hata hivyo halijawekwa wazi na uongozi wa Yanga.

Mzambia Zulu alitua nchini usiku wa kuamkia Jumanne, ikiwa ni miongoni mwa mapendekezo yaliyoainishwa na kocha mpya wa timu hiyo, George Lwandamina kama sehemu ya harakati za kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mzunguko wa pili na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

Baada ya Lwandamina kumalizana na Zulu, sasa amegeukia kwa mshambuliaji wa zamani wa Zesco, Kalengo kwa ajili ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.

Kalengo mwenye miaka 31, alijiunga na AC Leopards, Januari mwaka huu akitokea Zesco kwa dau la Dola 70,000 (Sh 153.3 milioni), huku akiwa analipwa mshahara wa Dola 10,000 (Sh21.8 milioni) kwa mwezi.

Mshambuliaji huyo anaweza kuwa suluhisho kwa safu yake ya ushambuliaji kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu, akiwa amefunga mabao 17 kwenye Ligi Kuu Congo ambayo AC Leopards inaongoza ikiwa na pointi 41 ilizozipata kwenye mechi 17.

Hata hivyo, Yanga inaweza kutumia nguvu ya ushawishi ya Lwandamina ili kumnasa Kalengo ambaye amekuwa na uhusiano mzuri naye.

Lwandamina aliyeanza kazi Jumatatu, ndiye alimruhusu Kalengo kujiunga na AC Leopards alipokuwa Zesco United, klabu ambayo mchezaji huyo aliichezea kabla ya kutimkia Congo.

 

Kipa Agyei apigwa pingu miezi 12

Simba, jana ilimtia pingu kwa mwaka mmoja kipa Daniel Agyei, huku ikishikwa kigugumizi cha kutaja mchezaji gani wa kigeni atakayeachwa ingawa imekuwa ikivumishwa kuwa ni kiungo Mussa Ndusha kutoka DRC.

Agyei aliyetua nchini juzi, alisaini mkataba huo katika ofisi za mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Medeama kumalizika.

Hata hivyo, pamoja na Agyei kusaini, Simba bado imeendelea kusita kutangaza mchezaji yupi atakayeachwa ili kumpisha kipa huyo kama kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinavyoeleza kwa wachezaji wa kigeni kuwa saba.

Kanuni zinataka kila klabu inayoshiriki ligi kusajili idadi ya wachezaji wasiozidi saba wa kigeni kwa ajili ya kuwatumia kwenye michezo ya ligi hiyo.

Kwa usajili wa Agyei, inamanisha kuwa Simba inatakiwa ipunguze mchezaji wa kigeni kutoka kwenye orodha yake baada ya kuwa nao wanane.

Wachezaji saba wa kigeni walioko Simba ni; Janvier Bokungu, Mussa Ndusha (DRC), Vincent Angban, Frederick Blagnon (Ivory Coast), Juuko Murshid (Uganda), Method Mwanjali (Zimbabwe) na Laudit Mavugo kutoka Burundi.

Ofisa habari wa Simba, Haji Manara aliliambia gazeti hili jana kuwa, ndani ya kipindi kifupi wataweka wazi usajili wao na mipango ya timu yao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu. “Kila kitu kimekwenda vizuri na klabu itatoa tamko kuhusu masuala ya usajili na mengineyo. Usajili tuliofanya ni mzuri na kwa kiasi kikubwa tunaamini utaisaidia timu yetu,” alisema. Manara.