Usiku wa deni haukawii kupambazuka

Muktasari:

Kwa nyakati tofauti jana, mashabiki hao kila mmoja alimtambia mwenzake, huku wale wa Yanga wakidai mechi hiyo ni sawa na ya kujipima nguvu kwani wao wanacheza na mabingwa wenzao Afrika siyo Simba. 

Dar es Salaam. Wakati mashabiki wa Yanga wakiikebehi Simba na kudai mechi yao ya leo ni sawa na kujipima nguvu kwani wao wamezoea kucheza na mabingwa wa Afrika, Simba imejibu mapigo na kusema wajiandae kulia.

Kwa nyakati tofauti jana, mashabiki hao kila mmoja alimtambia mwenzake, huku wale wa Yanga wakidai mechi hiyo ni sawa na ya kujipima nguvu kwani wao wanacheza na mabingwa wenzao Afrika siyo Simba.

“Unajua tumezoea kucheza na mabingwa wa Afrika, hata Simba wanajua, sema ndiyo hivyo mtu mzima hawezi kufa ‘kibudu’ kesho (leo) atakufa na tai shingoni,” alitamba katibu wa kundi la ushangiliaji la Wakali wa Terminal, Steven Mwakilema .

Simba imejibu mapigo hayo na kuiambia Yanga kwamba fowadi yao ya mwendokasi isubiri kupata pancha jioni hii, huku wakisisitiza mapema watakuwa Taifa (uwanjani) kuiunga mkono timu yao, ambayo kwa asilimia 100 wanaiamini itaifunga Yanga na kutwaa ubingwa.