Miezi 11 kipindupindu kikiua watu 71; Mbeya, Songwe yaongoza kwa vifo

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Takwimu hizo za Januari hadi Novemba zinaonyesha mkoa wa Mbeya umekuwa na wagonjwa 710 na vifo 14 huku Songwe ikiwa nao wagonjwa 538 na vifo vinne.

Dar es Salaam. Watu 3,739 wameugua na wengine 71 kufariki dunia kutokana na kipindupindu katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, huku mikoa ya Mbeya na Songwe ikiongoza kwa vifo.

Takwimu hizo za Januari hadi Novemba zinaonyesha mkoa wa Mbeya umekuwa na wagonjwa 710 na vifo 14 huku Songwe ikiwa nao wagonjwa 538 na vifo vinne.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu jana aliitaja mikoa mingine iliyoathirika zaidi kuwa ni Morogoro (320 na vifo 11), Dar es Salaam (320 na vifo vitano) Iringa (332 na vifo tisa), Kigoma (314 na vifo vinne). “Takwimu zinatuonyesha bado maambukizi mapya ni tishio kwani kuna ongezeko la idadi ya mikoa na halmashauri zinazotoa taarifa za wagonjwa japokuwa idadi imepungua mwishoni mwa mwaka,” alisema.

Ummy alisema takwimu za tangu mwaka huu uanze zinaonyesha ongezeko la ugonjwa ambapo mikoa 17 ilitoa taarifa za kuwapo kwa wagonjwa.

Hata hivyo, waziri alisema mikoa saba haikuripoti kuwa na ugonjwa huo ikiwamo Mwanza, Shinyanga, Arusha, Lindi, Kagera, Simiyu, Kilimanjaro na Mtwara.

“Nchi yetu inaelekea katika majira ya mvua ambazo zinaweza kuongeza kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu, hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa,” alisisitiza.

Waziri huyo aliwataka wananchi kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo ya makazi, kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kuwasafisha watoto waliojisaidia.

“Mamlaka za maji zilizopo nchini zihakikishe upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi, kunywa majisafi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na kupoa,” alisema.

Ugonjwa wa kipindupindu unachangiwa pia na kutokuwa na vyoo bora, huku ofisa mtendaji wa Kijiji cha Humekwa kilichopo Chamwino mkoani Dodoma, Ashrey Myogoya akisema kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira yenye kaulimbiu “usichukulie poa nyumba ni choo” imesaidia kwa kuwa mpaka sasa kaya zote 349 zina vyoo vilivyoboreshwa. Mkazi wa kijiji hicho, Cecilia Isaya alisema choo chake amekijenga kwa gharama ya Sh55,000.

“Si gharama kubwa nimetumia kwani baadhi ya vifaa nimenunua lakini vingine nimetengeneza mwenyewe ikiwamo matofali,” alisema.