Miezi 6 ya mvua yaja,mbinu za radi zatajwa

Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetangaza kuanza mvua kubwa kati ya Novemba hadi Aprili mwakani wakati huo huo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza mbinu za kujikinga na radi.


Geita/Dar. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikitangaza kuanza kwa mvua kubwa za juu wa wastani kuanzia mwezi ujao hadi Aprili 19, 2019, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limezungumzia namna ya kujikinga na radi kwenye makazi ya watu.

Akitoa utabiri wa mvua za msimu jijini Dar es Salaam jana, mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi aliitaja mikoa itakayopata mvua hizo kuwa ni Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, Kusini mwa Morogoro, Lindi na Mtwara.

Dk Kijazi alisema mvua hizo zinaweza kusababisha madhara kwa binadamu yakiwamo ya vifo, uharibifu wa miundombinu pamoja na hasara hasa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji.

Alisema utabiri huo ni kwa mikoa inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi kujihadhari na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo zinazotarajiwa kuanza wiki ya pili ya Novemba.

Wataalamu wazungumzia radi

Wakati mara nyingine mvua huambatana na radi, wataalamu wa umeme wameshauri wananchi waangalie mifumo ya waya za umeme mara kwa mara majumbani mwao.

Juzi radi ilisababisha vifo vya wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Emaco Vision iliyopo mjini Geita waliopoteza maisha wakiwa darasani,

Mtaalamu wa Tanesco mkoani humo, Charles Msangi aliliambia Mwananchi jana kuwa, uwepo wa waya uitwao ‘earth’ kwenye nyumba husaidia kuzuia radi isilete madhara kwa binadamu na badala yake huingia ardhini. “Siwezi kusema moja kwa moja kama nyumba haitadhurika, lakini ukiwa umeweka huo waya tunaita ‘earth rod’ unazuia radi, hata ikitokea inaenda ardhini lakini inategemea na ukubwa wa radi yenyewe,” alisema Msangi.

Waya huo unaelezwa kuwa huzuia madhara ya radi inayopiga kwenye waya wa umeme na kusababisha madhara kwa binadamu na si ile inayopiga kutoka juu moja kwa moja na kushuka ardhini.

Pamoja na mtaalamu wa umeme kuzungumzia namna ya kuepuka madhara yatokanayo na radi, Mwananchi limebaini kuwa shule iliyopigwa na radi juzi na kusababisha vifo vya wanafunzi haijawahi kuwa na huduma ya umeme.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Octavian Laurian alisema eneo ilipo shule halijafikiwa na huduma hiyo.

Maziko ya waliofariki dunia

Akizungumzia mazishi ya wanafunzi waliopoteza maisha, Mwalimu Laurian alisema wapo waliozikwa jana na wengine watazikwa kesho.

“Shule inashirikiana kwa karibu na familia ili kufanikisha maziko ya wapendwa wetu hawa,” alisema.

Akizungumzia hali ya majeruhi, kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Moses Simon alisema wanaendelea vizuri na tayari wanafunzi 14 kati ya 23 waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo wameruhusiwa kurejea nyumbani.

“Tumebaki na majeruhi tisa wanaoendelea na matibabu, saba ni wanafunzi na walimu wawili na (mwalimu) mmoja ana majeraha makubwa kwa sababu mwili wake ulipata majeraha makubwa ya moto,” alisema Dk Moses.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Mji wa Geita, Laurent Singano na Majaliwa Majaliwa waliiomba Serikali kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kujikinga na radi ili kuepuka madhara ya namna hiyo.

Singano alisema ni vyema kama kuna kifaa cha kuzuia radi kupiga kwenye majengo kikahamasishwa kwa wananchi kukinunua ili waweze kukifunga kwenye nyumba zao.

“Sijawahi kusikia kama kuna kifaa cha kuzuia au kujikinga na radi ni vyema kama kipo tukaelezwa,” alisema Singano.