Dk Miguna apeleka kampeni za NRM Uingereza

Muktasari:

  • Miguna ambaye amesema atatua Nairobi Jumatatu ya Machi 26 aliwasili Uwanja wa Ndege wa Heathrow Alhamisi saa 12.30 jioni kwa ajili ya ziara ambayo itamwezesha kutoa mhadhara

Mwanasheria machachari na ambaye amejitangaza kuwa Jenerali wa Vuguvugu la Kitaifa (NRM) Miguna Miguna amepeleka kampeni za "kuikomboa Kenya" nchini Uingereza.

Miguna ambaye amesema atatua Nairobi Jumatatu ya Machi 26, aliwasili Uwanja wa Ndege wa Heathrow Alhamisi saa 12.30 jioni kwa ajili ya ziara ambayo itamwezesha kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Oxford na kukutana na Wakenya wanaoishi London.

Taratibu za kiusalama ili kupata idhini zilicheleweshwa kwa sababu zisizojulikana hadi saa 3:30 usiku na wakati wote huo alikuwa akiwaahakikishia wenyeji wake kwamba kila kitu kiko kiko salama.

"Jiunge na Dk Miguna Miguna katika tukio hili kujihusisha, kujadili na kufikiria njia nyingi, zinazofaa, ngumu na za haraka za kuwaongoza Wakenya wanaoteseka kufikia uhuru," unasomeka mwaliko wa tuki.

"Mkutano huu ni wazi kwa Wakenya wote wenye mapenzi mema ambao wanataka kushiriki kwa dhati na Dk Miguna Miguna. Hebu tueneze neno hebu tusonge mbele. Huko hakuna gia ya kurudi nyuma."

Tukio hilo la Chuo Kikuu cha Oxford liliandaliwa na Kitivo cha Sheria, kwa mujibu wa mwanasheria. Kwa mujibu wa waandaaji, tukio hilo liliuzwa kwa wanafunzi kwa dakika 30.

Leo (Ijumaa), amepangwa kuhudhuria mahojiano kadhaa na vyombo vya habari vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kipindi cha asubuhi kwenye Shirika la Utangazaji la BBC.

Dk Miguna, ambaye alipuuzilia mbali mpango mpya wa ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga, anasema ataendelea na harakati zake za upinzani.