Miguna amlaumu Odinga kwa yanayomkuta Dubai

Muktasari:

Ingawa waziri mkuu huyo wa zamani hajatoa maoni yoyote hadharani kuhusu kuondolewa nchini kwa Miguna na kusafirishwa hadi Dubai, alijaribu kumwokoa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumatatu jioni.


Nairobi, Kenya. Sinema juu ya hatima ya mwanasheria machachari Dk Miguna Miguna bado inaendelea na kwa mara ya kwanza amemtupia lawama kiongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa Raila Odinga kwa kushindwa kumsaidia kurejea Kenya.

Katika taarifa yake aliyoituma kutoka Dubai, Falme za Kiarabu alikosafirishwa kwa nguvu na serikali, Miguna Jumamosi alimshutumu Odinga kwa kufanya karamu na watesi (wa mwanasheria huyo).

“Raila Odinga hawezi na hapaswi kukaa akifurahia Sikukuu ya Pasaka na wadhalimu huku mtu aliyesimamia kiapo chake cha kuwa rais wa watu “anauawa” na walewale waliomwibia ushindi katika uchaguzi uliopita na ambao wameua na kuwatia vilema wafuasi wake,” alisema.

Ingawa waziri mkuu huyo wa zamani hajatoa maoni yoyote hadharani kuhusu kuondolewa nchini kwa Miguna na kusafirishwa hadi Dubai, alijaribu kumwokoa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumatatu jioni.

Ripoti zinaonyesha Odinga aliondoka kwenye uwanja wa ndege baada ya juhudi za kutafuta ufumbuzi, ikiwemo ya kumpigia simu Rais Uhuru Kenyatta, kugonga ukuta.

Serikali, vyanzo vinasema, ilisisitiza kwamba Miguna lazima asalimishe pasipoti yake ya Canada kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Raila ambaye ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na ambaye amekubali kushirikiana kufanya kazi na serikali ya Kenyatta kwa ajili ya uponyaji wa nchi na umoja, alihudhuria kwa muda kusikiliza kesi juu ya uraia wa Miguna katika Mahakama Kuu.

Miguna amewahimiza wafuasi wake kumtaka Raila achukue hatua kwa sababu mateso yote anayopata ni matokeo ya kiapo alichomsimamia.

Pia amewataka wafuasi wake kuandamana na kuishinikiza serikali kuheshimu amri za mahakama na imruhusu kurejea nyumbani.

“Kusanyeni makundi makubwa ya watu waandamane, pigeni kelele na mdai kwamba haki zangu za kuzaliwa, kikatiba na kisheria ziheshimiwe na zizingatiwe,” alisema.

“Waheshimu amri za mahakama; nirejeshewe pasipoti yangu ya Kenya au nipewe mpya; ulinzi na usalama wangu uwepo.”

"Naomba kuokolewa kutoka Dubai, niruhusiwe kuondoka kwa usalama na kuingia kwenye nchi nilikozaliwa ya Kenya bila kukawia,” alisema.

"Mzaliwa wa Kenya hawezi kuzuiwa kuingia kwenye nchi aliyozaliwa. Sijawahi kuukana uraia wangu. Mahakama zimethibitisha na zimetambua uraia wangu."

Dk Miguna pia aliomba apatiwe huduma ya matibabu haraka akidai kemikali aliyodungwa wakati anasafirishwa inazidi kuathiri afya yake.

“Ni lazima nimwone dokta au tabibu na nifanyiwe vipimo vya kujua aina ya kemikali,” alisema.