Mikoa 12 nchini inavyonufaika kampeni ya kuwamilikisha ardhi wanawake vijijini

Muktasari:

Tayari wanawake 2,000 wameshanufaika, changamoto kibao zatajwa

Wanawake ni jeshi kubwa. Huo ni usemi maarufu miongoni mwa wanawake wanaposhiriki shughuli za kampeni zinazohitaji ushirikiano wa pamoja.

Hata kwenye suala la maendeleo ya kiuchumi, wanawake ndilo kundi kubwa linaloshiriki shughuli nyingi za kiuchumi hususan biashara ndogondogo ambazo ndizo zinashikilia nguvu ya uchumi katika jamii.

Hata hivyo, kundi hilo linakabiliwa na changamoto kubwa linapokuja suala la maendeleo ya kiuchumi kupitia rasilimali ardhi.

Hii ni kwa sababu mila na desturi za jamii nyingi nchini zinamuweka pembeni mwanamke inapofika suala la kumiliki ardhi.

Oxfarm wajitosa

Shirika lisilo la kiserikali la Oxfarm limeliona hilo na kuanzisha kampeni maalumu ya kuwawezesha wanawake, hasa vijijini ili wamiliki ardhi kwa kupatiwa hati miliki.

Kampeni hiyo inaendeshwa kupitia taasisi ya Urasimishaji wa Ardhi Vijijini (Rudi) kwa ufadhili wa Oxfarm na inatekelezwa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita, Mwanza, Mtwara, Lindi, Arusha, Manyara, Tanga, Morogoro, Dar es Salaam na Dodoma.

Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, kampeni hiyo inaendeshwa katika vijiji 12 vya wilaya za Shinyanga na Kahama mkoani Shinyanga pamoja na Maswa mkoani Simiyu ambapo kila kijiji kinapatiwa Sh4.5 milioni kwa ajili kuandaa na kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Meneja mradi wa Rudi, Stepheno Mpangala anasema hadi sasa kampeni hiyo imewawezesha wanawake 2,000 kutoka vijiji 12 vya wilaya hizo kumiliki ardhi kisheria.

Akitoa taarifa wakati wa mkutano wa wadau wa maendeleo uliofanyika jijini Mwanza kujadili mpango wa kitaifa wa umilikaji wa ardhi, Mpangala alisema kampeni hiyo iliyoanza mwaka 2012 imewawezesha wakulima zaidi ya 4,000 katika vijiji hivyo kumiliki ardhi.

Changamoto umiliki ardhi

“Mila na desturi za makabila mengi nchini zinamtenga mwanamke katika umiliki wa ardhi. Familia nyingi zimeingia kwenye migogoro pale baba anapofariki dunia na kumuacha mama na watoto wa kike kutokana na ndugu kutwaa ardhi,” anasema Mpangala.

Meneja huyo anasema kupitia kampeni ya Rudi, wanawake wakiwemo wajane na watoto wao wa kike wanamilikishwa ardhi na kupewa hati za kisheria na hivyo kuepuka kunyang’anywa na ndugu.

“Wanawake wakipatiwa hati miliki za ardhi wataondokana na hatari na migogoro inayohusu ardhi pindi wenza au wazazi wao wanapofariki dunia,” anasema.

Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Thomas Tukay anataja gharama za kupima ardhi na kutoa hati kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili kampeni hiyo.

Changamoto nyingine ni mwamko mdogo wa jamii katika masuala ya kupima ardhi pamoja na baadhi ya wanasiasa kuingilia mchakato wa kurasimisha ardhi.

Mwanamke na viwanda 2025

“Mpango wa Serikali ya Tanzania yenye uchumi wa kati ifikapo 2025 utafanikiwa iwapo jeshi kubwa la wanawake litawezeshwa kushiriki na kumiliki uchumi kupitia rasilimali ardhi,” anasema Mpangala.

Anasema kupitia ardhi, wanawake watazalisha mazao ya chakula na biashara zitakazotumika kama malighafi kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.

Ofisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Vivian Christian anasema kampeni hiyo inayotekelezwa katika vijiji vitatu wilayani humo itawezesha wananchi 378 kupata hati miliki.

“Halmashauri pia imeandaa bajeti maalumu itakayofanikisha utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vingine vinne itakayofanikisha uandaaji na utoaji wa hati miliki kwa wananchi 500,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisi Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Tukay anasema mradi wa huo umefanikisha utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vya Nyida, Nduguti, Ihalo, Welezo na Nsalala ambapo hati 361 za kumiliki ardhi zimetolewa.

Meneja mradi kutoka shirika la Oxfam, Boninventure Kagaye anasema urasimishaji wa ardhi utawawezesha wananchi vijijini kutumia rasilimali hiyo kukopa fedha za mitaji kutoka taasisi za fedha ili kufanisha na kuendesha miradi ya maendeleo.

“Ardhi ni utajiri ambao haujatumika kuinua maisha ya wananchi vijijini kulinganisha na mijini kutokana na kukosa nyaraka za kisheria zinazokubalika kwenye taasisi za fedha, kampeni hii itaondoa tatizo hilo,” anasema Kagaye.

Pamoja na wananchi kuhamasishwa kushiriki mpango wa matumizi bora ya ardhi utakaowawezesha kupata hati miliki za ardhi yao, ni vyema Serikali ikahakikisha huduma ya kupima ardhi kwa kuwafikia wananchi hadi vijijini. Gharama ya kupima ardhi na muda wa kuandaa na kukabidhi hati kwa wananchi navyo vinatakiwa kupunguzwa.