Mikoa 14 yaanza kampeni upimaji VVU

Muktasari:

Desemba mosi wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani itafanyika tathmini ya upimaji VVU kwa mikoa yote nchini

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi sasa mikoa 14 imeanza kutekeleza kampeni ya kitaifa ya kupima virusi vya ukimwi (VVU) kwa hiyari, pamoja na kuanza mapema matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi (ARV) kwa watakaogundulika kuwa na maambukizo.

Amesema hadi kufikia Septemba mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kigoma na Manyara ilikua imeanza kutekeleza kampeni hiyo.

Ameitaja mikoa mingine kuwa ni Mbeya, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Tabora na Tanga.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo katika hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, mwaka huu.

Aliwataka wakuu wa mikoa ambayo bado haijaanza kutekeleza kampeni hiyo waanze mara moja.

“Kwa kutambua umuhimu wa kampeni hii, ifikapo Desemba mosi wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani tutafanya tathmini ya utekelezaji kwa mikoa yote nchini. Kwa msingi huo nisisitize wadau wote wenye mapenzi mema na nchi hii wasaidie katika utekelezaji wa kampeni hiyo,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakuu wa mikoa hiyo 14 na akawataka waendelee kuhimiza wananchi kwenye maeneo yao hasa wanaume wawe tayari kutambua afya zao kuhusu maambukizo ya VVU.

Juni 19 Majaliwa alizindua kampeni ya kitaifa ya kupima kwa hiyari VVU jijini Dodoma ijulikanayo kama “Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi”, ambayo inawalenga Watanzania wote kupima na kutambua afya zao hususan wanaume ambao hawajitokezi kwa wingi kupima na kutambua afya zao.

“Wanaume wengi tumekuwa tukiwatumia wenza wetu kutambua kama tumeathirika au la. Tunakaa majumbani tunasubiri tu, ukimuona mwenza wako anarejea kutoka kliniki akiwa mwenye furaha na wewe unajipa matumaini kuwa umesalimika. Sasa wanaume wenzangu tubadilike, tuanze kuchukua hatua za kupima na kutambua afya zetu,” alisisitiza.