Mikopo elimu ya juu ikusanywe kwa ‘smartcard’

Muktasari:

Mfumo huo ambao tayari unatumika nchini Kenya, huhifadhi kumbukumbu za mlengwa kupitia nyaraka zake mbalimbali ikiwamo pasi ya kusafiria, hivyo humwezesha kurejesha mkopo akiwa nchi yoyote duniani.

Dar es Salaam. Jumuiya ya Taasisi za Mikopo ya Elimu ya Juu Afrika (AAHEFA) imezishauri nchi wanachama kutumia mfumo wa smartcard ili kukabiliana na changamoto ya ukusanyaji wa mikopo kwa wanafunzi waliohitimu elimu ya juu na kuwezesha utunzaji kumbukumbu za walengwa.

Mfumo huo ambao tayari unatumika nchini Kenya, huhifadhi kumbukumbu za mlengwa kupitia nyaraka zake mbalimbali ikiwamo pasi ya kusafiria, hivyo humwezesha kurejesha mkopo akiwa nchi yoyote duniani.

Akizungumza katika kongamano la nchi nane zinazojadili njia sahihi ya kuifanya mikopo ya fedha kwa ajili ya elimu ya juu kuwa endelevu na kuondokana na utegemezi serikalini, Rais wa jumuiya hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini Kenya (HELB), Charles Ringera alisema mfumo huo unaambatana na ukusanyaji wa taarifa za walengwa.

Alisema lazima mlengwa ajulikane ni nani, anatoka wapi na baada ya kumaliza elimu yake anafanya kazi sehemu gani au anatengeneza ajira wapi na atalipaje.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Simon Msanjila alisema lengo la kuondokana na utegemezi kwa Serikali ni kwa bodi za mikopo kuwa na fedha ambazo zinaweza kukopesha kwa wanafunzi sawa na zile zinazorudi kutoka kwa waliokopa.

“Baadhi ya wanafunzi wakishamaliza kusoma wanakwenda kufanya kazi nje ya nchi inakuwa vigumu katika ukusanyaji, hivyo tutatoka na kauli ya pamoja ili tuweze kukusanya mikopo waliko kupitia mfumo mpya,” alisema Profesa Msanjila.