Mikopo yatesa wafanyabiashara - Ndesamburo

Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo

Muktasari:

Ndesamburo alisema hayo wakati akizindua mradi wa mashine ya kusaga na kukoboa wa kikundi cha Vision Kata ya Njoro.

Moshi. Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amesema kuna wimbi la wafanyabiashara wanaofilisiwa na benki kutokana na mikopo.

Ndesamburo alisema hayo wakati akizindua mradi wa mashine ya kusaga na kukoboa wa kikundi cha Vision Kata ya Njoro.

Alidai kupigiwa simu nyingi na wafanyabiashara wanaouza nyumba na viwanja ili kuokoa visiuzwe kwa mnada.

“Katika biashara yoyote siri ya maendeleo ni nidhamu ya matumizi ya fedha. Msikope bila mpangilio.

“Unakopa unaweka mpaka rehani nyumba. Kina mama wamepoteza mali zao. Serikali badala ya kuwafundisha wananchi nidhamu ya kukopa, inahamasisha wakope,” alidai Ndesamburo.

“Nahubiri hili kwa kuwa  wenzangu wengi wako kwenye matatizo ya mikopo. Nyumba ‘zinakwenda’.  Kila siku napokea simu siyo chini ya 10 watu wanauza nyumba zao.

“Hao wanaouza ni watu ambao walikuwa wanatembea na Mercedes Benz (gari la kifahari). Sisemi msikope lakini unapokopa uwe na sababu za msingi ambazo umezipangilia siyo kuongeza mke,”  alisisitiza Ndesamburo.

Pia, alitoa msaada wa Sh2 milioni ili kutunisha mfuko wa kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka jana.