Mikosi yazidi kumwandama Manji, Serikali yamnyang’anya shamba

Muktasari:

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa shamba hilo pamoja na jingine la kampuni ya Amadori lililopo Kigamboni lenye ukubwa wa ekari 5,400 ambalo pia limefutiwa umiliki, yatapangiwa matumizi mengine.

Dar es Salaam. Mwaka wa majanga. Ndivyo unavyoweza kuutafsiri mwaka huu kwa kuangalia masaibu ambayo yamemwandama mfanyabiashara maarufu nchini, Yusufu Manji baada ya jana Serikali kutangaza kulifuta shamba lake lenye ukubwa wa ekari 714, lililopo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa shamba hilo pamoja na jingine la kampuni ya Amadori lililopo Kigamboni lenye ukubwa wa ekari 5,400 ambalo pia limefutiwa umiliki, yatapangiwa matumizi mengine.

Lukuvi alisema mashamba hayo yamenyang’anywa na Serikali kwa sababu hayakuwa yanaendelezwa na aliwaonya wananchi wasiyavamie na watakaokamatwa watashtakiwa.

Mikasa ya Manji

Hatua hiyo dhidi ya Manji imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kupoteza udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu kutokana na kutohudhuria vikao zaidi ya sita na vikao vya kamati vya maendeleo ya Halmashauri ya Temeke zaidi ya vitatu.

Septemba 6, Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo aliwaambia wanahabari kuwa wameamua kumuondoa Manji kwenye nafasi ya udiwani kwa kukosa sifa.

Manji ameupoteza udiwani huo akiwa amekaa mahabusu kwa karibu miezi miwili kutokana na kesi ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa inayomkabili.

Manji na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa baada ya kukutwa na jora la vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni pamoja na mihuri ya jeshi hilo.

Kesi hiyo ilikuja wakati akiwa anakabiliwa na mashtaka mengine ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin aliyosomewa Februari 17, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Klabu ya Yanga, alianza kuingia katika misukosuko Februari 8, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumtaja kuwa miongoni mwa watu 67 wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na biashara au matumizi ya dawa za kulevya.

Mbali na Manji, watu wengine maarufu waliotajwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima.

Februari 9, Manji aliripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam ambako wafuasi wa Yanga walifurika kituoni kabla ya kutawanywa na polisi.

Wakati Manji akiwa na kesi hiyo, wafanyakazi 25 wa kampuni yake ya Quality Group walikamatwa wakidaiwa kutokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini huku Manji naye akisubiriwa kuunganishwa nao kwa madai ya kuajiri wageni wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Aprili 19, wafanyakazi 16 wa kampuni hiyo raia wa India, walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja au kulipa faini ya Sh22 milioni baada ya kupatikana na hatia kwa mashtaka matano ikiwamo kufanya kazi nchini kinyume cha sheria na kuzuia maofisa Uhamiaji kutimiza majukumu yao.

Juni 24, Manji alimwomba radhi Rais Magufuli kutokana na kesi aliyoifungua akidai kupewa haki ya uwekezaji katika eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam.

Manji alikuwa ameshinda zabuni iliyotangazwa na Manispaa ya Kinondoni mwaka 2005, kwa ajili ya uwekezaji wa eneo hilo karibu na Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay.