Milioni 300 zachangwa kutunisha mfuko wa Ukimwi

Muktasari:

Katika uzinduzi huo, taasisi mbalimbali zilialikwa na kuuchangia mfuko huo zaidi ya Sh340 milioni.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu amezindua Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF) na kusema mahitaji ya Dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARVs) nchi ni makubwa huku wafadhili wakiwa wamepunguza misaada kwa Tanzania.

Akizindua mfuko huo jana, Samia alisema vipaumbele vya wafadhili vinabadilika siku hadi siku hivyo watanzania hawatakiwi kusubiri misaada wasiyokuwa na uhakika nayo.

Katika uzinduzi huo, taasisi mbalimbali zilialikwa na kuuchangia mfuko huo zaidi ya Sh340 milioni.

Alisema takwimu zinaonyesha kwamba watu milioni 1.5 nchini wanaishi na virusi vya Ukimwi na kwamba kutokana miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) wote wanatakiwa kuanza kutumia ARVs.

“Sasa hivi kila anayegundulika kuwa na virusi vya Ukimwi anatakiwa kuanza kutumia ARVs  tofauti na zamani matumizi ya dawa hizo yalizingatia kinga za mwili,” alisema.

Alisema kutokana na mwongozo huo, mahitaji ya dawa hizo yanaendelea kuwa makubwa.

“Naomba taasisi na watu mbalimbali wachangie kusaidia mfuko huu ili kujenga uwezo wetu wa ndani katika mapambano dhidi ya Ukimwi,” alisema.