Mimba jinamizi linalokwamisha ndoto ya maskini kupigiwa kura

Muktasari:

  • Takwimu za Mkoa wa Geita zinaonyesha wanafunzi 218 wamekatiza masomo tangu 2013

Licha ya Serikali kusisitiza wanafunzi watakaopata mimba kutoendelea na masomo, tatizo la mimba shuleni linaongezeka na kukatisha ndoto zao za maisha.

Hali hiyo inakwamisha ndoto za jamii maskini kwamba ipo siku ingetoa kiongozi kwa kupigiwa kura, lakini hatua hiyo inasababisha iendelee kuongeza wapiga kura kwa sababu hawatakuwa na sifa zitokanazo na elimu.

Katika Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita, takwimu zinaonyesha wanafunzi 33 wamepata ujauzito kipindi cha Julai 2016 hadi Juni mwaka huu.

Akitoa taarifa juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Carlos Gwamagobe alisema miongoni mwa wanafunzi hao, 19 wanasoma sekondari na 14 shule za msingi.

Alisema kesi zote 33 zimeripotiwa polisi, lakini inasikitisha zinapofikishwa mahakamani hukosa ushahidi.

“Tunajitahidi kusimama na kupeleka kesi polisi, lakini mwisho wa siku mashahidi wanadanganywa na kupindisha ushahidi tatizo linaanzia ngazi ya familia,” alisema.

Alisema kumekuwa na mchezo wa wakuu wa shule, walimu, watendaji wa vijiji, polisi na wazazi ambao hushirikiana na kumaliza tatizo kimya kimya kesi inapofikishwa mahakamani.

Mmoja wa wanafunzi wa waliopata ujauzito ambaye alikuwa anasoma Shule ya Msingi Bukwimba, alisitisha masomo ikiwa ni miezi miwili kumaliza elimu yake baada ya kupata mimba inayodaiwa alipewa na mwalimu.

Mwanafunzi huyo alisema alifanya mapenzi na mwalimu huyo kwa nyakati tofauti na alikuwa akimpatia kati ya Sh2,000 hadi 10,000, ambazo alikuwa akitumia kununulia nguo, mafuta na mahitaji mengine binafsi. Hata hivyo, mwalimu anayedaiwa kumpa mimba mwanafunzi huyo, alikanusha na kwamba, kilichofanyika ni chuki kati yake na mwalimu mwingine ambaye wameungana na mwalimu mkuu kumbambikia kesi.