Mimba ya mwanafunzi yaibua mazito

Muktasari:

Mwenyekiti atuhumiwa kupokea fedha ili kumaliza kesi, mwenyewe asema itikadi za kisiasa zinatumika vibaya kumchafua

Geita. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ihega, Kata ya Bukoli, Wilaya ya Geita mkoani hapa, Zawadi Makenzi anatuhumiwa kupokea Sh500,000 ili kumaliza kesi ya kijana aliyempa mimba mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Bukoli.

Mwenyekiti huyo anadaiwa kuwakutanisha walezi wa mwanafunzi huyo na kijana anayedaiwa kumpa mimba na kukubaliana kumaliza kesi hiyo kwa kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bukoli, Devat Stanslaus alisema taarifa za mwenyekiti huyo alizipata kwa wananchi na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria ili hatua za sheria zichukuliwe dhidi yake.

“Nililetewa malalamiko hapa ofisini na baadhi ya wananchi ya mwenyekiti kukubali kumaliza kesi ya mtu aliyempa mimba mwanafunzi kwa kuimaliza kienyeji, mwenyekiti hana uwezo wa kusikiliza kesi kama hii na kuitatua na wazazi ili isifike kwenye vyombo vya sheria. Hili ni kosa kubwa,” alisema Stanslaus.

Mtendaji huyo alisema inadaiwa mwenyekiti huyo baada ya kupewa fedha alitoa Sh300,000 akawapa wazazi wa binti huyo na 200,000 alibaki nazo na kuimaliza kesi hiyo kifamilia.

Alipotafutwa kufafanua juu ya madai hayo, Makenzi alikana na kudai yanayosemwa yanatokana na itikadi za kisiasa kwa kuwa yeye ni mwenyekiti kupitia Chadema.

“Sijapewa fedha zozote huu ni mgogoro wa kisiasa na unasababishwa na watu wa CCM kwa kuwa hawataki niwe mwenyekiti,” alisema Makenzi.

Hata hivyo, alikiri kufikishwa polisi kwa tuhuma hizo na kusema lengo lake ni kuona mwanafunzi huyo anasaidiwa.

Akizungumza na gazeti hili, mwanafunzi aliyepata ujauzito alisema kwa sasa hana taarifa za mwanaume aliyempa mimba na kwamba hali hiyo imetokea baada ya kukutana na mwenyekiti kwa mazungumzo pamoja na bibi ambaye ni mlezi wake.

Mwanafunzi huyo alisema umasikini wa kipato kwenye familia ni sababu iliyochangia kujiingiza kwenye vitendo vya ngono akiwa mwanafunzi.

“Nilikutana na Dulla nikiuza uji jioni kutokana na bibi yangu kuwa ni mzee na nilikuwa nikitoka shule napika uji wa ulezi nauza gengeni ili nipate fedha za chakula na mahitaji ya shule, yangu na mdogo wangu na alikuwa mmoja wa wateja wangu, shida zikanifanya niingie kwenye mapenzi kwa kuwa alikuwa ananipa pesa,” alisema mwanafunzi huyo.

Bibi wa binti huyo, Maua Said alisema mwenyekiti huyo alimuita kwenye kikao cha majadiliano, lakini hana uhakika kama kijana huyo alitoa fedha za kumaliza kesi hiyo kwa kuwa baada ya kikao hajawahi kumuona.

Licha ya kukiri kukutana na mwenyekiti huyo, bibi Maua hakutaka kueleza kwa kina sababu zilizomsukuma kufanya majadiliano na kiongozi huyo wala hatima ya ujauzito na elimu ya mjukuu wake.

Sakata hilo limekuwa gumzo katika kitongoji hicho na viunga vyake.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliagiza wanaowapa mimba wanafunzi wasakwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.