Mishahara yafyeka bajeti ya Tamisemi

Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene

Muktasari:

Bajeti hiyo iliwasilishwa jana na Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene aliyesema kuwa kati ya fedha hizo, Sh4.54 trilioni zitatumika katika matumizi ya kawaida (mishahara na matumizi mengineyo). 

Dodoma. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imewasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2017/18 ikiomba kuidhinishiwa Sh6.5 trilioni huku kiasi kikubwa cha fedha Sh 4.07 trilioni zikienda kwenye mishahara.

Bajeti hiyo iliwasilishwa jana na Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene aliyesema kuwa kati ya fedha hizo, Sh4.54 trilioni zitatumika katika matumizi ya kawaida (mishahara na matumizi mengineyo).

Kwa mujibu wa bajeti hiyo Sh1.78 trilioni zinaombwa katika kugharamia miradi ya maendeleo.

Wakati Tamisemi ikiomba fedha hizo, mwaka 2016/17 Bunge liliidhinisha Sh6.02 trilioni huku mishahara ikitafuna Sh3.7 trilioni, sawa na theluthi mbili ya bajeti, na Sh1.6 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, hadi kufikia Februari mwaka huu (miezi minne kabla ya mwaka wa bajeti kumalizika), fedha zilizopokelewa na wizara hiyo zilikuwa ni Sh3.55 trilioni (Sawa na asilimia 59.1) ya bajeti yote iliyoidhinishwa na Bunge.

Watumishi hewa

Simbachawene alisema watumishi 13,369 ambao ni watoro na waliofariki dunia wameondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali.

Alisema kati ya idadi hiyo, 541 walikuwa ni wa sekretarieti za mikoa na watumishi wa serikali za mitaa ni 12,828 ambao waliisababishia Serikali hasara ya Sh25.4 bilioni.

Hata hivyo, alisema Sh 2.7 bilioni sawa na asilimia 11 zimerejeshwa serikalini.

“Ufuatiliaji unaendelea ili kuhakikisha fedha zilizobaki zinarejeshwa na kuwachukulia hatua watumishi waliohusika na upotevu huo,” alisema Simbachawene.

Alisema watumishi wasio waadilifu wameendelea kuchukuliwa hatua.

Elimu bila malipo

Kuhusu suala la elimu bure, Simbachawene alisema kuna tofauti kati ya elimu bure ya msingi na elimu ya msingi bila malipo.

“Wananchi wanakuwa wazito kujitolea hata nguvu zao katika kuchangia shughuli mbalimbali zinazohusu elimu kwa kisingizio kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa elimu msingi bure,” alisema.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, asasi zisizo za kiserikali, wadau wengine wa elimu, wazazi na walezi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha uwepo wa miundombinu muhimu ya shule kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali, msingi na sekondari,” alisema.

Maoni ya kamati ya Bunge

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jasson Rweikiza alishauri wakati akitoa maoni ya kamati hiyo kuwa Serikali itoe fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati.

Alisema kufanya hivyo kutaziwezesha halmashauri kulipa madeni ya wazabuni na wakandarasi kwa wakati na hivyo kuepusha ongezeko la madeni katika miradi inayotelekeza.

“Mikoa iandae vipaumbele vichache kulingana na uwezo wa bajeti na kusimamia kikamilifu utekelezaji wake, badala ya kuwa na msururu wa vipaumbele ambavyo havitekelezeki kutokana na ufinyu wa bajeti,” alisema Rweikiza.