VIDEO: Mitambo, vifaa vya kunyanyua Mv Nyerere vyawasiri Ukara

Muktasari:

  • Mitambo hiyo imewasili katika gati ya Bwisya kusaidia kazi ya kunyanyua, kugeuza na kukivuta kivuko hicho kilichopinduka Septemba 20

Ukara. Mitambo na vifaa maalum vya kunyanyua, kubeba na kuvuta vitu vizito imewasili katika gati ya Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe tayari kufanya kazi ya kunyanyua na kugeuza kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka katika ziwa Victoria.

Mpaka kufikia jana wataalam wa uokoaji na masuala ya majini walifanikiwa kukilaza ubavu kivuko hicho ambacho awali kililala kifudifudi tangu kilipopinduka Septemba 20.

Mitambo na vifaa hivyo vimewasili asubuhi ya leo vikiwa ndani ya meli mbili kubwa binafsi za Mv Nyakibaria ya kampuni ya Mkombozi and Fisheries na Mv Orion II inayomilikiwa na kampuni ya Kamanga Ferry, zote za jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Isaac Kamwelwe alisema mitambo na vifaa hivyo vitarahisisha kazi ya kunyanyua, kugeuza na kukivutia ufukweni kivuko hicho.

"Mitambo tunayotegemea kupata kutoka GGM ina uwezo na nguvu zaidi kulinganisha na tuliokuwa tukiutumia awali," alisema Kamwelwe ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Ajali hiyo ya kupinduka Mv Nyerere imesababisha vifo vya watu 227 ambao miili yao imeopolewa, huku wengine 41 wakiokolewa wakiwa hai.

Serikali imetoa ubani wa Sh1.5 milioni kwa kila familia ya aliyekufa katika ajali hiyo, huku walionusurika wakipewa pole ya Sh1 milioni kila mmoja.