Miundombinu kikwazo cha uchumi wa viwanda Pwani

Muktasari:

Kati ya mambo wanayoya-fanya vijana ili ndoto hiyo itimie ni pamoja na kutumia kila fursa wanayoiona mbele yao ikiwemo kupata mafunzo ya ujasiriamali na mikopo inayotolewa na Serikali na taasisi mbalimbali za kifedha.

Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa inaimba wimbo wa Tanzania ya viwanda, kundi la vijana haliko nyuma katika kuhakikisha hilo linatekelezeka.

Kati ya mambo wanayoya-fanya vijana ili ndoto hiyo itimie ni pamoja na kutumia kila fursa wanayoiona mbele yao ikiwemo kupata mafunzo ya ujasiriamali na mikopo inayotolewa na Serikali na taasisi mbalimbali za kifedha.

Miongoni mwa vijana hao ni wale wa Kisarawe, Mkoa wa Pwani ambao baada ya kusikia mradi wa kuwezeshwa kiuchumi vijana ulio-fika katika eneo lao hawakulaza damu. Mradi huo unaojulikana kwa jina la YEE unaotekelezwa na Shirika la Plan International katika wilaya 10 ambapo kwa Mkoa wa Pwani wilaya za Kibaha na Kisarawe zimehusishwa.

Kwa Kisarawe peke yake, umewezesha vijana zaidi ya 1,200 kupata elimu ya ujasirimali na ufundi mbalimbali ukiwemo wa magari, kushona nguo kwa chere-hani, mapishi, mapambo na ufundi umeme.Katika utekelezaji wake vijana hao walifundishwa kwa muda wa miezi sita, mitatu ilikuwa darasani na mitatu kivitendo, huku kukiwa na ushirikiano mkubwa wa Mamla-ka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta). Baada ya kumaliza, vijana hao wamegawiwa vifaa vya kuanzia kazi huku mitaji ya fedha wakiipata kupitia mikopo inayo-tolewa na halmashauri ambapo wapo waliopata hadi Sh5 milioni.

Robert Adam, kiongozi wa kikundi cha Vijana Tukiwezeshwa Tunaweza kilichopo kitongoji cha Marumbo wilayani Kisarawe, anasema juhudi zote hizo zinaweza kuwa bure kama miundombinu haitakuwa rafiki kwake.

Miundombinu anayozungumzia Adam anayejihusisha na ufundi wa kushona nguo ni pamoja na barabara akisema ili kufika katika kijiji hicho inampasa mtu kupanda pikipiki kwa Sh2,000 kutoka kilipo kituo cha basi.

“Unajua huku kwetu barabara ni mbaya, hivyo hata mabasi hayafiki, sasa inabidi uchukue boda eneo ambalo basi linaishia ili kufika,’’ anasema Adam.

“Pia kwa kuwa hakujachangamka kibiashara malighafi ikiwemo vitambaa nyuzi za kushonea na vifaa vingine yatupasa kuvifuata Kariakoo jijini Dar es Salaam na hapo hutulazimu kutumia si chini ya Sh6,000 kwa safari moja.”

Anasema jambo hilo linasababisha wanapopata oda ya kushona nguo za haraka kushindwa kutokana na muda mwingi kuutumia barabarani.

Kwa upande wa umeme, Mwanaidi Malela ambaye ni mmoja wa wanakikundi anasema awali walikuwa wakitumia taa ya kuchaji, ambapo kila siku iliwalazimu kutoa Sh500 kwa ajili ya kuchajiwa.

Hata hivyo anaushukuru uongozi wa Halmashauri ya Kisarawe baada ya kupata malalamiko yao uliwapatia mkopo ambao pia waliutumia kununulia mashine ya ‘sola’ na sasa wanautumia japokuwa mvua zikinyesha mfululizo inakuwa tabu kuchaji.

“Yaani hapa nishati ya kuaminika ni umeme tu, kwani sola nayo huwa na ufanisi zaidi kunapokuwa na jua kali, mvua zikinyesha mfululizo nguvu yake inapungua na hivyo tunashindwa kumaliza kazi za watu kwa muda tuliopanga,” anasema Mwanaidi.

Kuhusu mawasiliano ya simu, Halima Khamis ambaye alijifunza masuala ya kupika na kupamba, anasema mitandao mingi ya simu haijafika katika eneo lao hilo la Marumbo.

Kitendo hicho, Halima anasema kinawafanya kukoswa hewani na wateja wao na kujikuta wanakosa kazi nyingi pale zinapotokea, na kuambulia zile za karibu ambazo mtu anawafikia kwa kutembea kwa miguu.

“Hili suala la mawasiliano kwetu ni changamoto kubwa ukizingatia tayari tuna mikopo tunayotakiwa kuirudisha na tunategemea kazi ili tupate hela. Sasa unapokosekana hewani ni wazi kwamba urudishaji wa mikopo utakuwa shida, tunaomba kampuni za simu zifike huku kwani nasi mawasiliano kwetu ni muhimu,” anasema.

Viongozi wao wanasemaje?

Tatizo hilo linamvuta mwandishi wa makala hii hadi kwa diwani wa Marumbo, Mayasa Yange ili kujua nini mikakati yake katika kuhakikisha wanafikiwa na miundombinu hiyo ili kuwaondolea adha vijana hao wajasiriamali.

Katika maelezo yake, Mayasa anasema suala la barabara tayari Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), wameshawafikishia kero hiyo na waliwajibu kuwa walikuwa wanasubiri kipindi cha masika kiishe ndipo waanze kushughulikia.

Kwa upande wa mitandao ya simu, anasema mnara uko Maneromango, eneo ambalo ni karibu na kata yake japo haufikishi mawasiliano kwao, lakini kutokana na malalamiko ambayo tayari ameyafikisha kwenye vikao vya halmashauri ana imani tatizo hilo litatatuliwa.

Kuhusu umeme, anasema vijiji vitatu kati ya sita tayari vimeshafikiwa na umeme na vilivyobaki kikiwemo cha Marumbo, shughuli ya kuweka alama kwa ajili ya nguzo imekamilika na taarifa alizonazo ni kwamba mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo ana shughuli nyingine mkoani Tanga ambapo akiimaliza atahamia kwao.

Faida kwa wananchi Kisarawe

Pamoja na kuwepo kwa changamoto kadha wa kadha, katibu tawala wa Wilaya ya Kisarawe, Mtela Mwampamba anasema kwa sasa vijana wengi waliokuwa wakikaa vijiweni wamebadilika na kuanza kujishughulisha.

Anasema kutokana na mafunzo hayo wametoa mikopo kwa vikundi vilivyoundwa japokuwa kuna wachache ambao hawajaendelea na wengine hawajahifadhi vifaa walivyopewa na kurudi kwenye shughuli zao za zamani ikiwemo kilimo.

Mambo kama hayo anasema yameisukuma halmashauri kuitisha kikao cha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo madiwani ili kujadili na kuona nini hasa tatizo walifanyie kazi, mradi huo uwe endelevu kwao. Ofisa maendeleo ya Vijana wa wilaya hiyo, Dalidali Rashidi anasema anachoona kwa vijana wengine ‘kuingia mitini’ ni mwamko wa wazazi na jamii zinazowazunguka katika kuwaunga mkono kutumia huduma zao.

“Kwa halmashauri tumekuwa tukijitahidi kuwapa tenda mbalimbali ikiwemo kunapokuwa na shughuli kama za mwenge, sare wanatushonea wao kwani nia yetu ni mikopo tunayowapa irudi. Hivyo hata kipaumbele chetu ni kuwapa kazi waliokopa kwetu,” anasema.

Ili kuhakikisha wanabadilika pia viongozi, jamii na wazazi wanapaswa kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kupata mafunzo hayo na kuyafanyia kazi ukizingatia kwamba wengi wao bado wana umri ambao wanapaswa kuongozwa kimaisha na wazazi au walezi.

Katika kusaidia mradi huo kuendelea kuwa endelevu pamoja na kukaribia kufikia ukingoni mwishoni mwa mwezi huu, anasema halmashauri itaendelea kutoa mikopo kwa wale waliojiunga katika vikundi na mpaka sasa vikundi 68 vimeshaundwa kutokana na YEE.

Kwa upande wao, madiwani akiwemo wa Kisarawe ambaye kata yake inatajwa kufanya vizuri katika mradi huo, Abel Mudo anasema moja ya mafanikio hayo ni kutokana na kujitolea muda kuwafuatilia na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo kuwasaidia kwa kuwa Serikali pekee haiwezi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Marumbo, Sadi Kibwana anashukuru tangu vijana hao wapate mafunzo, huduma ambazo walikuwa wakizifuata Kisarawe mjini sasa wanazipata hapohapo kijijini.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa vijana wa Kisarawe, wenzao wa Kibaha imekuwa neema ya kubadilisha maisha.

Mmoja wa wanufaika aliyejitambulisha kwa jina la Kulwa Omar (20), anaishukuru YEE kumwezesha kupata ajira katika kiwanda cha kubangua korosho, ambako anafanya kazi ya ufundi akiwa ni tegemeo katika masuala ya umeme kiwandani hapo.

Kwa upande wake, Salama Ally anashukuru mradi huo kubadilisha maisha yake kutoka kuuza ubuyu na karanga hadi kumiliki saluni na kuwaomba wadau wengine kufanya miradi kama hiyo kwa kuwa huu unaelekea ukingoni.

Hata hivyo pamoja na mradi kuhitaji kuwafikia asilimia 10 ya watu wenye ulemavu katika wilaya hizo 10, imeonekana kuna changamoto kuwafikia huku Serikali ikibainisha baadhi ya sababu ikiwemo mazingira na kushindwa kuifikia mikopo.

Ofisa maendeleo kwa Vijana Halmashauri ya Kibaha, Pudensian Domel anasema pamoja na kutenga asilimia mbili ya fedha za mikopo kwa ajili ya walemavu, kundi hilo limeshindwa kutumia fursa hiyo kutokana na riba kuwa kubwa.

Pudensian anasema pamoja na mradi huo kuwafikia hadi walemavu ambao walipaswa kuunda vikundi vitakavyofaidika na mikopo ya halmashauri, wameshindwa kufanya hivyo kwa kuhofia riba.

“Jambo wanalolitaka wenzetu hawa ni kupewa mikopo hiyo pasipo na riba, jambo ambalo haliwezekani kwani pamoja na waziri wa Tamisemi (Selemani Jafo) kutoa agizo hilo katika moja ya mikutano hatuwezi kufanya hivyo kwa kuwa hatujapata mwongozo kimaandishi huku chini,” anasema ofisa huyo.

Hatua hiyo, anasema imesababisha kati ya Sh37 milioni zilizotengwa kwa ajili ya mikopo, Sh2 milioni pekee ndizo zimetumika hadi sasa.