Mjadala Muungano wamkwaza Majaliwa

Muktasari:

Jenista aliomba mwongozo wa Spika akitaka kiti kutenda haki kuzuia mjadala usio na afya bungeni ukiwemo wa Muungano.


Dodoma. Mjadala uliosababisha baadhi ya wabunge kususia kikao juzi, umemfanya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa ya moyoni wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya ofisi yake jana.

Majaliwa amesema kwamba mjadala ulioibuka juzi kuhusu Muungano haukuwa na afya na hatarajii kuona hali hiyo ikijirudia.

Juzi wabunge wa upinzani kutoka Zanzibar walitoka ukumbini baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kuagiza mjadala usio na afya kwa Muungano usijadiliwe hadi atakapojibu mwongozo ulioombwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge), Jenista Mhagama.

Jenista aliomba mwongozo wa Spika akitaka kiti kutenda haki kuzuia mjadala usio na afya bungeni ukiwemo wa Muungano.

“Mheshimiwa Spika, nieleze masikitiko yangu juu ya mjadala ulioendelea jana, sikuridhika na mjadala wa jana,” alisema Majaliwa wakati akianza kuhitimisha hotuba yake.

“Najua ziko hoja lakini mjadala wa jana (juzi) kwa namna nilivyojifunza ni mgogoro wa mtu na mtu, kundi na kundi, jambo ambalo halileti tija wala afya hapa kwetu.”

Majaliwa alisema anatambua kuwa yapo mapungufu, lakini viongozi wote wameapa kuusimamia Muungano na kwamba jukumu la wengine ni kuunga mkono ili kuulinda.

“Tunajua kwamba kutokana na kuingia madarakani na Serikali ya sasa ina miaka miwili, yapo maboresho na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, yapo maboresho. Maboresho haya yanaweza kuathiri mfumo wa kawaida ambao tulianzanao na ambao tunaumaliza kupitia vikao tulivyo navyo,” alisema.

Alisema hawazuii mbunge kuuliza jambo ili apate ufafanuzi, lakini pia “haturuhusu mtu na mtu watumie Bunge kupotosha ukweli wa mambo”. Awali juzi, mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Hussein Salim alisema changamoto za Muungano hazijatatuliwa akitoa mfano wa sukari ya Zanzibar kuzuiwa kuuzwa Tanzania Bara, kauli iliyoibua mjadala.

Na Majaliwa alidokezea suala hilo akisema suala hilo lilitokana na sukari.

Waziri mkuu alisema chanzo cha malumbano ni suala la uagizaji sukari kutoka nje ya nchi ili kufidia upungufu uliopo nchini.

Alisema katika kutimiza azma hiyo, Serikali haiangalii kama mwagizaji ametoka Tanzania Bara au Zanzibar.

Waziri Mkuu alitoa mfano, akisema mwaka 2016 upungufu uliojitokeza ulikuwa tani 140,000 lakini waagizaji waliopewa vibali walikuwa wawili kutoka Zanzibar, watatu kutoka Bara na kiwanda cha sukari cha Mahonda kilipewa kibali cha kuagiza tani 390.

Alisema mwaka 2017, upungufu ulikuwa tani 140,000 na waliopewa vibali walikuwa wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Bara, lakini kwa mwaka huu upungufu ni tani 135,000.

Waziri mkuu alisema tofauti na awali, safari hii waliopewa vibali ni wenye viwanda ili waagize sukari kutoka nje.

“Kwa hiyo, jambo hili la sukari lisivuruge Muungano wetu,” alisema Majaliwa.

Alisema nia ya Serikali ni kuzalisha sukari ya kutosha ili Taifa lijitegemee.

Majaliwa aliwataka mawaziri wa biashara wa Zanzibar na Bara wawe makini ili sukari inayoagizwa nje isije kufurika katika soko la ndani kwa sababu gharama za uzalishaji sukari ya ndani ni kubwa.

Alisema viwanda vilivyopo ni sita, vitano vikiwa Bara na kimoja Zanzibar, lakini havina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya bidhaa hiyo.

Demokrasia nchini

Baada ya kuhitimisha hotuba hiyo, mawaziri walijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wabunge.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba hiyo alimuomba Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kuchukua hatua stahiki kwa vyama vyote ambavyo havitaki kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria na utaratibu ili kusaidia mfumo wa vyama vingi uwe halisia unaoendana na matakwa ya kisheria.

Kuhusu kuzuiwa maandamano, Mhagama alisema wabunge wa upinzani wamelalamika kwamba yanazuiwa wakati ni suala la kikatiba.

Alisema maandamano yanaratibiwa kwa sheria ya usalama chini ya polisi, na Katiba haiwezi kuchukuliwa tu kuruhusu maandamano bila sheria kufuatwa.

“Niulize tu, tukiamka hapa siku moja asubuhi kila mtu aamue kuandamana kwa sababu Katiba imesema, nadhani haitakuwa sawa. Naomba vyama viheshimu Katiba na sheria,” alisema Mhagama.

Kuhusu fedha nyingi kutumika katika uchaguzi mdogo, alisema hakuna demokrasia isiyo na gharama.

“Kama jimbo la uchaguzi lipo wazi lazima tufanye uchaguzi, ndiyo maana nasema ni gharama ya demokrasia,” alisema.

Operesheni uvuvi haramu

Naye Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliomba kibali kwa Waziri Mkuu na kwa Spika ili wakubali aendeshe semina Aprili 21 aeleze jinsi gani rasilimali zilizoko katika sekta ya uvuvi zinavyofujwa na watu wasilolitakia mema Taifa.

“Lakini yapo mambo madogo ambayo yameshauriwa na wabunge katika uboreshaji na mimi sina tatizo na uboreshaji. Ndiyo maana katika Bunge lile nilisema mbunge yeyote mwenye hoja, mwenye jambo lolote atuletee sisi tutachukua hatua,” alisema.

Alisema tayari wamewasimamisha kazi watumishi tisa waliohusika kwa namna moja kuhujumu au kujinufaisha binafsi katika operesheni hiyo.

Alisema ametoa maelekezo kwa maofisa wake kuacha kuwakamata watu wanaobeba samaki kwa ajili ya kitoweo cha nyumbani ambao awali, walikuwa wakikamatwa katika mabasi.

Hata hivyo, aliwaonya watu kutotumia mwanya huo kutumia mabasi ya abiria kwa ajili ya kufanya biashara.

Mauaji, utekaji

Kuhusu matukio ya utekaji, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba aliagiza kufanyika uchunguzi wa ndani ili kupata taarifa na wataendelea kutoa taarifa kadri zitakavyopatikana.