Mjadala mzito wa mawaziri waibuka

Rais John  Magufuli

Muktasari:

Hata hivyo, Mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa alisema uteuzi alioufanya Rais si lazima umaanishe kuwa umefanywa kwa lengo fulani na kwamba kinachotakiwa ni kusubiri kile ambacho atakifanya.

Dar es Salaam. Mjadala wa uwezekano wa kufanyika kwa mabadiliko ya mawaziri umezidi kukolea baada ya Rais John Magufuli kumteua Dk Abdallah Possi kuwa balozi na hivyo kuweka uwezekano wa mbunge huyo wa kuteuliwa, kuachia uwaziri.
Hata hivyo, Mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa alisema uteuzi alioufanya Rais si lazima umaanishe kuwa umefanywa kwa lengo fulani na kwamba kinachotakiwa ni kusubiri kile ambacho atakifanya.
Hadi sasa, Baraza la Mawaziri linaundwa na mawaziri 19 na manaibu 14 na alifanya mabadiliko mara mbili; ya kwanza alipomhamisha Profesa Makame Mbarawa kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwenda Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na ya pili alipotengua uteuzi wa Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Kutenguliwa kwa Kitwanga kulimfanya Rais amhamishe Mwigulu Nchemba kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani na hivyo kumteua mbunge wa Buchosha, Dk Charles Tizeba kuziba nafasi aliyokuwa akishikilia Mwigulu.