Mjamzito asimulia jinsi alivyookolewa

Grace Elisha

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi jana, Grace ambaye ni mama wa watoto wawili, Jenipher Madaraka (3) na Catherine Madaraka (2) alisema bila muujiza wa Mungu, angepoteza uhai katika ajali hiyo.

Ukerewe. Grace Elisha (27), mjamzito wa miezi saba mkazi wa Kijiji cha Bwisya kilichopo Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe ni miongoni mwa manusura 41 wa ajali ya kivuko cha Mv Nyerere.

Akizungumza na Mwananchi jana, Grace ambaye ni mama wa watoto wawili, Jenipher Madaraka (3) na Catherine Madaraka (2) alisema bila muujiza wa Mungu, angepoteza uhai katika ajali hiyo.

Kivuko cha Mv Nyerere kilizama Alhamisi iliyopita saa 7:48 mchana kikiwa mita 50 kabla ya kutia nanga katika ghati la Bwisya. Hadi jana alasiri miili ya 224 ilipatikana.

“Nilitoka nyumbani kwangu asubuhi kwenda Bugolora kuhemea mahitaji ya nyumbani. Nikiwa njia kurejea nyumbani ndipo janga hili lilipotokea na kuangamiza watu wengi,” alisema Grace.

“Ikiwa inakaribia kutia nanga katika ghati ya Bwisya huku baadhi ya watu wakianza maandalizi ya kuteremka, ghafla meli iliyumba na nikajikuta nimetumbukia ndani ya maji.”

Alisema akiwa ndani ya maji, huku akijitahidi kujiokoa kwa kuogelea, alibamizwa mgongoni na pikipiki iliyorushwa kutoka ndani ya kivuko, hali iliyomsababishia maumivu na kupoteza nguvu na uwezo wa kujiokoa.

Kutokana na kutapatapa akipiga kelele kuomba msaada, mmoja wa abiria wa kiume ambaye naye muda huo alikuwa akijitahidi kujiokoa aliogelea hadi alipokuwa na kumwelekeza amshikilie mguu ili wajiokoe pamoja.

“Kutokana na hofu ya kifo iliyoniingia, nilijikuta nikimshika mguu kwa nguvu kiasi cha yeye kushindwa kuogelea. Kitendo hicho kilimfanya anipige teke kujiokoa asizame pamoja nami.

“Baada ya kuogelea na kusogea mbali kidogo kutoka nilipokuwa, mwanamume yule aliingiwa imani jinsi nilivyokuwa natapatapa majini nikiomba msaada. Alirejea nilipo na kunisihi nijikaze kusubiri waokoaji (wavuvi) ambao tayari walikuwa wameshaingia majini kuelekea kilipo kivuko.

“Nikiwa nimechoka na kuishiwa nguvu huku mawazo na hofu ya kifo yakianza kunijaa, ghafla nilimwona kaka Bishompa Sendema akiwa anatumia boya kuogelea kujiokoa. Nilipiga kelele nikimwita jina ndipo alipogeuka na kuniona natapatapa majini.”

Alisema kelele hizo zilimfanya Bishompa (36) kugeuza boya na kuogelea kumfuata. Alipomfikia alimtaka kujishikilia kwenye boya hilo.

“Alianza kuogelea kumfuata binti mwingine ambaye pia alikuwa akitapatapa majini na tumtaka pia ashikilie boya kwa nguvu. Tukiwa watatu kwenye boya, Bishompa akaogelea kumfuata mwanamume mwingine aliyekuwa akizama na kwa pamoja akatutaka kushikilia boya kwa nguvu,” alisema Grace.

Hivyo ndivyo Grace na wenzake wawili walivyookolewa na Bishompa ambaye hata hivyo, mama huyo anasimulia kwamba;

“Kutokana na kufanya kazi kubwa ya kuokoa watu watatu alianza kuishiwa nguvu kabla naye kuokolewa na boti za wavuvi waliokuwa wamefika tayari kutoa msaada.”

Akiwa katikati ya maji kabla ya kuokolewa, Grace alikuwa na mawazo mengi, “Wakati natapatapa huku nguvu zikiniishia, hofu ya kifo iliniingia nikaanza kuwaza jinsi ninavyowaacha watoto wangu ambao bado ni wadogo, mume wangu pamoja na mama yangu mzazi. Hata suala la kufa na mtoto wangu mwenye umri wa miezi saba tumboni pia liliniumiza sana moyoni.”

Amepoteza ndugu watatu

Licha ya furaha ya kunusurika aliyonayo, Grace alipata huzuni kubwa baada ya kupata taarifa za kupoteza shemeji zake watatu waliokuwamo kwenye ya kivuko.

“Ndani ya meli (kivuko) tulikuwa ndugu watano, nilikuwapo mimi, mama yangu mzazi pamoja na shemeji zangu watatu. Mama amepona kama mimi lakini shemeji zangu wote wamekufa.”