Mkakati wa kuifanya Dodoma ya kijani unavyosukwa

Muktasari:

Katika uzinduzi huo alitaka mpango huo wa upandaji miti uwe wa kudumu na kuwataka viongozi na wanaDodoma kuipokea kampeni hiyo kwa mikono miwili na kutoa kila aina ya ushirikiano ili kufikia lengo zuri lililokusudiwa.

Dar es Salaam. Desemba 22 mwaka jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu alizindua kampeni ya upandaji miti kulifanya Jiji la Dodoma kuwa wa kijani.

Katika uzinduzi huo alitaka mpango huo wa upandaji miti uwe wa kudumu na kuwataka viongozi na wanaDodoma kuipokea kampeni hiyo kwa mikono miwili na kutoa kila aina ya ushirikiano ili kufikia lengo zuri lililokusudiwa.

Kuhakikisha lengo hilo lililokusudiwa linafanikiwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeingia mkataba na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kusimamia ustawishaji miti mjini humo.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi anasema wamepanga kuwa na misitu ndani ya jiji jambo ambalo linawezekana kwa kuwa kuna waliofanya hivyo.

Anasema nchi mbalimbali zimefanya hivyo ambapo kuna makazi kidogo na misitu.

Wakati wa utiaji saini wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo alisema kwa kuwa Dodoma imeshakuwa makao makuu ya nchi anategemea kutakuwa na ongezeko la watu, hivyo shughuli nyingi za kiuchumi zinatarajiwa kwa muda mfupi ujao.

“Shughuli hizo zitasababisha kuwa na hali fulani ambayo itahitaji mazingiza yake yaboreshwe kuondoa hali ambayo inaweza ikachafua mazingiza na kuathiri afya za wakazi wa Jiji la Dodoma,” alisema Profesa Silayo.

Jiji, mkoa wamejipangaje?

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, Kunambi anasema wametenga takriban hekta 150 ambazo TFS wataanza upandaji wa miti.

Anasema kumekuwa na kampeni za kupanda miti miaka mingi, lakini miti hiyo haistawi hivyo hivi sasa hawatatumia neno kupanda miti, bali kustawisha miti.

“Unaposema kustawisha miti ni pamoja na shughuli yenyewe ya kupanda lakini na kuufanya mti ule uendelee, hivyo tutumie neno kustawisha miti kwani kupanda tu dhana yake ni kuipanda na kuiacha,” anasema Kunambi.

Anasema miti lazima ipandwe kwa mujibu wa sheria kwa kuwa hawataona haya kukataa au kumnyima mtu kibali cha upandaji.

Akizungumzia kuibadilisha Dodoma kuwa ya kijani, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge anasema upandaji wa miti ni muhimu kwa kuwa hata mvua zilizopita ziliwaletea madhara makubwa kutokana na uhadibifu wa mazingira hasa ukataji miti.

“Mkakati wa kutunza mazingira kwa kupanda miti una matokeo makubwa hapo baadaye, tumepanda miti Mzakwe, pia Udom na Nzuguni,”anasema Dk Mahenge.

Anasema suala la msingi ni kupanda mti na kuustawisha, na wamepanga kupanda miti milioni moja na nusu kila mwaka katika halmashauri na ifuatiliwe.

“Kama inapandwa miti kwenye kata wenyeviti wa vijiji washirikishewe, hivyo itakuwa ni jukumu la kata na kijiji kuhakikisha hiyo miti inastawi,” anasema.

Anasema baada ya miaka mitano kutakuwa na misitu na hali ya ukijani.

RC aitaja korosho

Pia jingine litakalowasaidia kuweka ukijani huo ni kilimo cha korosho katika wilaya za Mpwapwa, Kongwa, Chemba na Bahi ambako wananchi wamechangamkia kilimo cha zao hilo. “Zao la korosho ni la kibiashara, lakini ni dhahabu ya kijani kwa kuwa linatumia maji kidogo,” anasema Dk Mahenge.

Anasema kutokana na uwepo mdogo wa maji mkoani Dodoma wanapanda miti inayohitaji maji kidogo na kutumia msimu wa mvua za mwakani kupanda miti kila Jumamosi na Jumapili ili kuweza kuyatumia maji hayo.

Anasema Dodoma mjini itabadilika kwa kuwa inategemea kupata watu wanaofikia 420,000 na uwezo wake ni kuwa na watu 500,000.

Wananchi na mabadiliko

Ukiachana na mkakati wa kuibadilisha Dodoma kuwa ya kijani baadhi ya wananchi wanazungumzia mabadiliko wanayoyaona kuwa ni ya kutia matumaini.

Mkazi wa Dodoma, Jella Mambo anasema kuwa kumekuwapo na ongezeko la aina ya vyakula katika jiji hilo, lakini tatizo miundombinu bado haijakamilika vizuri kuweza kufika kila mahala.

“Naona mabadiliko makubwa katika wingi wa vyakula vinavyopatikana mjini hapa. Zamani tulikuwa tukitafuta matunda kama mapapai hakuna, lakini sasa ukifika kila eneo hakuna kinachokosekana tena kwa bei ya kawaida,” anasema Mambo.

Hata hivyo anasema kuna msongamano wa magari katika maeneo mbalimbali ya mji unaotokana na barabara kuwa ndogo na hivyo kutohimili mahitaji ya magari.

“Hali ya ulinzi ni imara lakini sasa unakuta ikifika saa 10 jioni wakati watumishi wa Serikali wanatoka kazini unakuta foleni kubwa katika barabara inayoelekea Dar es Salaam, kulikuwa hakuna maandalizi katika suala la miundombinu, ndiyo maana imekuwa hivyo,” anasema.

Mikakati ya kuondokana na jambo hilo, hata hivyo, imeshaelezwa na Kunambi kuwa jiji linatengeneza barabara pete ambazo zitakuwa zinauzunguka mji wa Dodoma na kuondoa foleni katikati.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisoile anasema mabadiliko katika jiji hilo yalianza kuonekana tangu Udom ilipoanzishwa kwa idadi ya watu kuongezeka, lakini wameongezeka zaidi baada ya Serikali kuhamia.

“Mwaka 2008 tulipokuja ukiwa na Sh10,000 hupati chenji kwa sababu ya mzunguko mdogo wa fedha, lakini baada ya kuja Udom kulikuwa na mabadiliko ambayo sasa yamekuja kuchagizwa kwa Serikali kuhamia Dodoma,” anasema. Anasema kumekuwapo na mabadiliko ya ongezeko la watu na pia kasi ya ujenzi wa nyumba imeongezeka na hayo yatabadilisha hali ya jiji hilo.

Anasema idadi ya watu inavyongezeka itasaidia ubunifu katika biashara na shughuli za kifedha.