Mkali wa rap, XXXTentacion auawa kwa risasi

Muktasari:

XXXTentacion alipigwa risasi na mtu aliyekuwa akimvizia wakati akitoka dukani


Broward.Mwanamuziki wa nyimbo za rap wa Marekani XXXTentacion, ambaye alipata umaarufu kwa haraka kupitia albamu zake mbili ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa na miaka 20.

Mwanamuziki huyo alipigwa risasi akiwa anatoka kwenye duka la kuuza pikipiki Kusini mwa Florida jana Jumatatu na mtu mmoja ambaye ilidaiwa alikuwa anamvizia.

Polisi wa Broward wanasema XXXTentacion, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Jahseh Onfroy, alikimbizwa hospitalini lakini akathibitishwa kufariki.

Alikuwa mara nyingi akielezwa kama mmoja wa wanamuziki wa rap wenye kuzua utata zaidi. Alikuwa pia amekabiliwa na mashtaka ya kumshambulia mpenzi wake.

Rapa huyo, ambaye alipata umaarufu kwa kupakia nyimbo zake katika mtandao wa SoundCloud, alikuwa anatazamwa na wengi kama kielelezo cha mtu kufanikiwa kupitia kipaji chake.