Mkapa: Kuna janga katika elimu nchini

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Rais Mstaafu Benjamin Mkapa (kushoto) akimwapisha Makamu Mkuu  mpya wa Chuo hicho, Prof Egid Mubofu (kulia) katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga chuoni hapo mwisho wa wiki.  Na Mpigapicha Maalum

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili, kwa Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu kuzungumzia mustakabali wa sekta ya elimu ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita.

Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi, utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Hii ni mara ya pili, kwa Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu kuzungumzia mustakabali wa sekta ya elimu ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita.

Novemba 11, akizungumza katika kongamano la wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Mkapa alisema Tanzania haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu.

Alisema kwa hali ilivyo, “Tunahitaji kufanya mapinduzi kwenye elimu.”

Janga katika elimu

Jana kwa mara nyingine, akizungumza katika hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula, Mkapa alisema kuna janga katika elimu.

“Ninaamini kabisa kwamba tuna crisis (janga) ninasoma katika magazeti, ninaletewa presentation (mawasilisho) kutoka sekta binafsi, walimu, private university (vyuo binafsi). Napata pia minong’ono kutoka kwa vyuo vya umma kwamba kuna (crisis) katika elimu,” alisema.

Mkapa ambaye pia ni mkuu wa chuo hicho, alisema aliwahi kuwa mhariri wa magazeti ya chama (Uhuru na Mzalendo) na baadaye ya Serikali (Daily News na Sunday News) na kwamba njia moja ya kujua mwenendo wa mambo ni kusoma barua kutoka kwa wasomaji.

“Nimeendelea kusoma magazeti sana mpaka mke wangu ananilalamikia. Lakini nyingi (barua za wasomaji) zinalalamika zinasema hivyo hivyo. Zinasema elimu yetu ina mushkeli,” alisema.

Alisema wapo watu wanaolalamika juu ya lugha, ratiba, ushirikiano, lakini pia juu ya ushirikishwaji wa wahitimu, wanaofanya kazi na wazazi ili kuamua Taifa linakwendaje katika elimu siku zijazo.

“Kwa nini ukisoma katika orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu wao katika 10 za kwanza ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za Serikali ni za watu binafsi? Kama Serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, kuna kasoro gani?”alihoji.

Alisema ni vyema kukaitishwa mdahalo wa uwazi ambao utashirikisha makundi yote na kusikia maoni yao badala kuwaachia wanataaluma pekee ambao wanaegemea kwenye ujuzi.

Alisema baadhi ya Watanzania wanamletea taarifa wanasema elimu ya nchini ni ya chini kuliko nchi za Kenya na Uganda, lakini hafahamu kama kuna ukweli juu ya jambo hilo.

Alisema ingekuwa ni vizuri kujiuliza kwa uwazi kama kuna tatizo na kama lipo ni kwa jinsi gani linaweza kusahihishwa ili kuongeza ubora wa elimu nchini.

“Naomba uisome tena hotuba yangu niliyoitoa siku ya convocation (kongamano la kitaaluma). Najua mtasema nimelalamika lalamika lakini na mimi ni raia bwana. Sina gazeti, sina NGO (asasi ya kiraia) kama Twaweza. NGO yenye jina langu, Benjamin Mkapa Foundation inashughulika na afya sio elimu… nimeona bora nitoe korongo langu mbele yenu wote,” alisema Mkapa.

Wadau na shaka kuhusu elimu

Kauli ya kiongozi huyo imekuja katika kipindi ambacho wadau wengi wa elimu wanautilia shaka mwenendo wa sekta ya elimu nchini.

Miongoni mwa shaka za wadau wa elimu ni pamoja na utekelezaji wa muundo mpya wa wanafunzi wa shule za msingi kusoma kwa miaka sita.

Jingine ni ukosefu wa vitabu kwa wanafunzi wa darasa la nne ambao wameshaanza kusoma kwa mtalaa wa muundo mpya wa miaka sita.

Mwananchi limebaini kuwa wanafunzi wa darasa la nne nchi nzima hawana vitabu vya kujifunzia, licha ya masomo kuanza tangu shule zilipofunguliwa mwanzoni mwa mwaka.

Gazeti hili lilidokezwa na baadhi ya walimu kwamba ukosefu wa vitabu hivyo unaongeza ugumu wa ufundishaji licha ya sababu nyingine.

‘’Mpaka sasa, wanasema wameelezwa watumie vitabu vya Kiingereza vinavyotumika katika shule binafsi maarufu kama ‘international schools’ kwa kuvitafasiri kwa Kiswahili jambo linalowawia vigumu.

“Mpaka mwezi huu wa tatu, hakuna vitabu na hawa wanafunzi watafanya mitihani ya kujipima Novemba mwaka huu. Sasa tunajiuliza itakuwaje ikiwa kwa sasa hawasomi kama inavyotakiwa,” alidokeza mmoja wa walimu.

Mwalimu mwingine alisema wanafunzi hao wakiwa darasa la tatu mwaka jana, baadhi ya vitabu vyao vilichelewa na vingine kutopatikana kabisa na kinachowatokea sasa ni awamu ya pili ya tatizo lilelile.

“Mwaka jana vitabu vilichelewa, sasa hivi navyo hakuna, sijajua mwisho wao itakuwaje. Kama hawatakuwa na msingi mzuri huku chini, huko mbele watapata matokeo mabaya,” alisema.

Hivi karibuni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alikaririwa na gazeti hili akisema hakuna mwanafunzi anayesoma sasa elimu ya msingi atakayekumbwa na utekelezaji na mfumo mpya.

Alisema wanafunzi wote walioko shuleni wataendelea kutumia utaratibu wa kawaida wa miaka saba, huku akisema Serikali bado haijakamilisha baadhi ya mambo muhimu ikiwamo yale yanayohusu miundombinu na walimu.

“Suala hili halitatekelezwa sasa na wanafunzi wote walioko shuleni watamaliza shule kwa kipindi cha miaka saba. Wakati ukifika tutatoa taarifa kupitia taratibu zilizopo,” alisema.

Walimu wataka vitabu

Baadhi ya wadau wa elimu wameitaka Serikali kusambaza vitabu vya mtalaa mpya kwa ajili ya kufundishia masomo ya darasa la nne, wanaojiandaa kufanya mitihani yao mwishoni mwa mwaka huu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kankwale, iliyopo Sumbawanga, Rukwa Abbas Kasela alisema hayo kwa kuwa mitalaa ya shule ya msingi imebadilika, Serikali kupitia wizara husika ina wajibu wa kutoa vitabu vinavyoendana na mabadiliko ya mitalaa hiyo.

“Mitaala imebadilika lakini vitabu vya kufundishia mitaala hiyo mpya haijafika hadi sasa, tunalazimika kuazima kwa shule binafsi. Sasa ifike wakati wizara ilete vitabu vya kufundishia mapema ili tuweze kuwasaidia wanafunzi wa darasa la nne wanaotarajia kufanya mitihani mwishoni mwa mwaka huu” alisema.