Mkataba kati ya NSSF na Azimio wakwamisha mradi wa nyumba 7000

MVUTANO NA MBIA WAKWAMISHA MRADI WA NSSF

Muktasari:

Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Godius Kahyayara amesema mradi huo umeshatekelezwa katika awamu mbili

Dar es salaam. Mvutano wa hisa kati ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Azimio, umeelezwa kuwa chanzo cha kuchelewa kwa mradi wa nyumba zaidi 7,000 zilizopo eneo la Dege Beach Kigamboni jijini Dar es salaam.

Hayo yalibainika leo Januari 20, 2018 katika ziara iliyofanywa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika eneo la mradi.

Awali Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Godius Kahyayara amesema mradi huo umeshatekelezwa katika awamu mbili ambapo nyumba 3,750 zimeshakamilika kati ya nyumba 7,160 za mradi mzima.

Amesema kwa mujibu wa mkataba huo, kampuni ya Azimio iliyotoa ardhi ya hekta 300 inamiliki hisa 55% huku NSSF iliyowekeza zaidi ya Dola 500 ikimiliki hisa asilimia 45.

Amesema mradi huo utakaogharimu dola za 544 za Marekani ulitarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu lakini haitawezekana kutokana na dosari za mkataba.

Baadhi ya wajumbe wa PAC wamehoji sababu ya Mkurugenzi wa kampuni ya Azimio kutoonekana kila anapotafutwa.

Mbunge wa viti maalum (CCM), Shaly Raymond amesema kuchelewa kwa mradi huo kutapandisha gharama kutoka Dola 544 milioni hadi zaidi ya 700 na kuhoji nani atakayelipa.

"Angalia hiyo meza kuu, mwekezaji hayupo wewe Mkurugenzi umekuja peke yako, wenzako wako wapi?" alihoji Shaly.

Naye mbunge wa viti maalum (CCM), Felister Bura amesema kama Azimio hataki kuonyesha ushirikiano, atafutwe mwekezaji mwingine."Tulipozungumza na mwekezaji huyu alikubali kupunguza hisa zake kwa sababu amewekeza kidogo. Kama anasumbua NSSF waangalie namna ya kupata mwekezaji mwingine,” amesema.

Akijibu hoja za wabunge hao, Profesa Kahyarara amekiri i kucheleweshwa kwa mradi, kwamba bado wanajadiliana na kampuni ya Azimio.

Alimtetea mwekezaji huyo akisema amekuwa na safari nyingi nje ya nchi na kwamba atakuwepo kwenye kikao cha January 26 ambapo mambo yote yatajadiliwa na kutolewa uamuzi.