Mkataba tata jengo la Mkuki waipasua kichwa Temeke

Muktasari:

Mei mwaka huu, halmashauri hiyo iliunda timu ya wataalamu kufanya ukaguzi wa kina na ndiyo iliyoamua kumuomba mthamini wa majengo kutoka serikalini ili abainishe gharama halisi ya ujenzi.

Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imekwama kumpata mthamini wa majengo kutoka serikalini ili kutathmini gharama za jengo la Mkuki ambalo mwekezaji ametumia Sh31 bilioni kujenga ghorofa tano badala ya 10 zilizokusudiwa.

Mei mwaka huu, halmashauri hiyo iliunda timu ya wataalamu kufanya ukaguzi wa kina na ndiyo iliyoamua kumuomba mthamini wa majengo kutoka serikalini ili abainishe gharama halisi ya ujenzi.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Nassib Mbaga alipoulizwa kuhusu mkataba huo na sababu za kushindwa kumpata mthamini kwa miezi mitano, alitupa mpira kwa mchumi wa manispaa hiyo, Edward Simon mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya uwekezaji, miradi na programu mbalimbali za maendeleo.

Simon alisema: “Tulikubaliana kumpata mthamini wa Serikali lakini hadi sasa uthamini haujafanyika. Ule mradi una meneja, tulikuwa naye kwenye ziara iliyofanyika Mei 3 palepale mkurugenzi alimpa jukumu aandae hiyo programu ya kuhakikisha tathmini hiyo inafanyika kwa kuwa yeye ni msanifu majengo.

“Kwa hiyo meneja bado hajatuambia ni mahali gani amekwama. Hadi kwenye taarifa ya Julai – Septemba alikuwa hajakamilisha mchakato huo wa kumpata mthamini, ila nitamtafuta nizungumze naye pengine siku mbili hizi kunaweza kuwa na jambo jipya.”

Juhudi za kumpata meneja mradi huyo, Jimmy Ringo zilishindikana baada ya simu yake kuita kwa muda mrefu bila kupokea.

Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo alithibitisha hivi karibuni kuwa kuna mambo ambayo yanaonekana yamekiukwa hivyo kuwa tofauti na mkataba ikiwamo idadi ya ghorofa na kuongezwa kinyemela ukubwa wa eneo la ujenzi.

“Halmashauri imeunda timu ya kufanya ukaguzi. Pia, tumemuomba mthamini wa majengo wa Serikali ili atusaidie tujiridhishe na thamani ya jengo kwa sababu mwekezaji ametuambia ametumia Sh31 bilioni hadi sasa,” alisema Chaurembo.

Meya huyo alisema tatizo la kwanza ni mwekezaji, Showmax Dubai General Trading LLC, kushindwa kukamilisha ujenzi wa ghorofa tano tangu uliposainiwa mkataba mwaka 2008, na tatizo la pili ni mwekezaji kujenga eneo kubwa zaidi ya ramani iliyokuwapo.

Vilevile, meya huyo amelalamikia uongozi uliopita kwa kukubali kuingia mkataba wa miaka 33 kwa viwango maalumu vilivyowekwa katika kipindi chote cha mkataba bila kuwapo kipengele cha kufanyia marekebisho kulingana na thamani ya fedha ya wakati husika.

Kwa mujibu wa mkataba huo, halmashauri itakuwa inalipwa na mwekezaji kodi ya pango ya Dola za Marekani 50,000 kwa miaka minane ya kwanza, halafu mwaka wa tisa hadi wa 15 kodi itakuwa Dola 80,000; mwaka wa 16 hadi 20 itakuwa Dola 100,000; mwaka wa 21 hadi 25 itakuwa Dola 100,000 na kati ya mwaka 26 na 33 kodi itakuwa Dola 150,000.

“Sisi tuliukuta mkataba huu ndiyo tupo tunaufanyia maboresho kwa jinsi tunavyoweza, maana safari bado ni ndefu. Ndiyo kwanza miaka nne bado miaka kama 29,” alisema.

Chaurembo alisema walioingia mkataba hawakuwa makini, kwani hawakuzingatia kuwa kiwango cha fedha huwa kinabadilika mwaka hadi mwaka, hivyo kwa kuwa mkataba ni wa miaka mingi ilibidi kuwe na kipengele kinachoeleza kuwa unaweza kubadilika kiwango chake kulingana na thamani ya fedha.

“Hatutegemei kwenye suala la upangishaji thamani ishuke. Wenzetu walioingia mkataba hawakuzingatia hayo sasa wametuweka kwenye hali ngumu inayotusumbua. Ila jambo la kushukuru ni kwamba mwekezaji ni mtu ambaye anakubali mazungumzo. Hilo la kodi tumezungumza naye na kukubaliana kwamba atatulipa kwa eneo mraba na pia amekuwa akilipa kodi hiyo hata kabla hajaanza kulitumia jengo lenyewe,” alisema.

Kuhusu mwekezaji kuzidisha eneo la ujenzi, Chaurembo alisema halmashauri imeona kuwa ni tatizo ambalo lilichangiwa na msimamizi ambaye hakuwa makini kwa sababu ndiye aliyetakiwa kutoa mwongozo.

Mkataba wake

Ripoti ya Baraza la Madiwani inaeleza kuwa jengo hilo lililopo Barabara ya Nyerere, limejengwa kwa mkataba wa ubia kati ya Manispaa ya Temeke na mwekezaji, kampuni ya Showmax Dubai General Trading LLC.

Kwa mujibu wa mkataba huo uliosainiwa Mei 12, 2008, mwekezaji alitakiwa kujenga, kuendesha na kuwarudishia majengo Manispaa ya Temeke iliyotoa ardhi ya ukubwa wa mita za mraba 23,976. Kampuni hiyo iligharamia ujenzi huo kwa Sh32 bilioni lakini imejenga jengo katika ukubwa wa mita za mraba 33,000 ikieleza kuwa lina ubora zaidi ya vile walivyotegemea kwa kuwa lina sehemu ya maegesho.

Ripoti hiyo inaonyesha mabadiliko ya ukubwa wa eneo la ujenzi, mwekezaji kujenga ghorofa tano badala ya 10 na viwango maalumu vya malipo ya pango kwa miaka 33 kabla ya manispaa kukabidhiwa jengo hilo, mambo ambayo yamesababisha mjadala mkali.

“Kwa mujibu wa mkataba, mwekezaji bado hajajenga ghorofa tano ili kukamilisha idadi ya ghorofa 10 zilizotajwa ndani ya mkataba, mkandarasi alipaswa kuwa amekamilisha ujenzi wa ghorofa 10 mnamo au kabla ya tarehe 12/4/2011 au muda mwingine uliokubaliwa na pande zote mbili,” inasema sehemu ya taarifa ya Baraza la Madiwani.

“Hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha mwekezaji kuomba kuongezewa muda ili kukamilisha kazi ya mkataba.”

Kamati ndogo ya menejimenti ilikutana Machi 6, 2015 na mwekezaji aitwaye Hasain Mohamed Gulam Hussein ambaye ndi ye mwenye kiapo cha uwakilishi wa kampuni ya Showmax Dubai General Trading LLC kuhusiana na masuala yote ya mradi na alieleza kuwa ujenzi bado unaendelea na aliahidi kuendeleza ujenzi huo kuanzia Julai mwaka huu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba ujenzi haujaanza na juhudi za kumpata mwekezaji ili azungumzie jambo hili hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa amesafiri nje ya nchi.