Mkataba wa Tanesco, Songas waguswa katika ripoti ya CAG

Muktasari:

  • Katika ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2016/17, CAG anasema kuna uwezekano kuwa Tanesco haikupata thamani ya fedha kwa mali zilizohamishiwa Songas, kiasi kwamba thamani ya hisa ilizopewa shirika hilo zinaweza kuwa za chini kuliko thamani halisi ya mali hizo.

 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameangazia mkataba kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Songas akishauri ufanyiwe tathmini upya.

Katika ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2016/17, CAG anasema kuna uwezekano kuwa Tanesco haikupata thamani ya fedha kwa mali zilizohamishiwa Songas, kiasi kwamba thamani ya hisa ilizopewa shirika hilo zinaweza kuwa za chini kuliko thamani halisi ya mali hizo.

CAG anasema alibaini eneo la Ubungo Complex lilihamishwa kwenda Songas mwaka 2004 wakati Songas ilipoanza kufanya kazi zake Tanzania. Kutokana na mkataba wa kuhamisha, uhamisho huo ulihusisha haki ya umiliki wa ardhi na mali zisizohamishika, umiliki wa mali zinazohamishika (pamoja na vipuli na injini ya kufua umeme -turbines), tafiti (intellectual properties) na haki yoyote kutoka kwa shirika la umeme ambayo itaiwezesha Songas kumiliki, kufanya kazi na kudumisha Ubungo Complex.

CAG anasema Tanesco ilipewa hisa 10,000 katika mtaji wa Songas na Songas ilichukua madeni ya Tanesco ambayo yalitumika kununulia injini nne za maji zilizopo eneo la Complex.

Kutokana na mkataba wa usimamizi kati ya Jamhuri ya Muungano na Benki ya Biashara ya Ulaya, mchango wa mtaji wa Tanesco na Shirika la Maendeleo la Mafuta Tanzania (TPDC) katika Kampuni ya Songas ni Euro 5 milioni, ambapo Shirika la Maendeleo ya Mafuta lilikuwa na hisa 20,000. “Hata hivyo, kulikuwa hakuna ushahidi unaoonyesha eneo la Complex na mali zake ambazo zilihamishwa kwenda kampuni ya Songas zilikokotolewa thamani yake kabla ya kuhamishwa,” anasema.

“Pia, hakuna kipengele katika makubaliano ya kuhamisha na mkataba wa mkopo kinachoonyesha kiasi cha mkopo uliochukuliwa na Songas uliotumika kununua injini za kufua umeme.”

Ripoti inaeleza mkataba wa usimamizi wa fedha ambao ulisainiwa kati ya Serikali, Benki ya Biashara ya Ulaya na Songas unaonyesha gharama ya mradi wa Songas ilikuwa ni Euro 392 milioni (sawa na Dola 346 milioni za Marekani kwa wakati ule).

Hata hivyo, anasema alibaini Serikali ilifanya uwekezaji mkubwa wa asilimia 73 katika mradi bila kuuthaminisha.

“Hakuna sehemu yoyote kwenye mkataba ambayo inaonyesha umiliki wa Serikali kwenye mradi licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali,” anasema.

Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia kipengele hicho cha ripoti ya CAG, meneja biashara wa Songas, Sebastian Kastuli alisema wanazijua taarifa hizo ila hawawezi kuweka utetezi wao kwenye vyombo vya habari.

“Tuna taarifa hiyo, lakini tungependa kujibu moja kwa moja kwa CAG na kwa Rais, kwa hiyo tusingependa kueleza kwa vyombo vya habari,” alisema Kastuli.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema kuna hoja atazijibu bungeni.