Mke wa Mugabe ataka mumewe ateue mrithi

 Mke wa Rais Robert Mugabe, Grace Mugabe

Muktasari:

Kauli hiyo ya Grace ni wazi imepokelewa kwa mshangao na wanasiasa walio wengi nchini humo hasa wale ambao tayari wameanza kupigana vikumbo kuwania kumrithi Mugabe.

Harare, Zimbabe. Mke wa Rais Robert Mugabe, Grace Mugabe amevunja desturi mojawapo kubwa ya Chama cha Zanu PF, kwa mshangao kwa kumtaka mumewe huyo mwenye umri wa miaka 93 amteua mrithi wake.

Mwanamama huyo ambaye ni mwenyekiti wa tawi la wanawake la Zanu PF alisema hayo jana alipokuwa akihutubia kikao cha Umoja wa Wanawake kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Harare.

Grace alijaribu kutumia Biblia katika rai yake alipozungumzia fumbo la Adonija aliyeandaa hafla ya kujitawaza yeye mwenyewe kwa kuwa mfalme baba yake alikuwa mgonjwa. Kichekesho ni kwamba hata Mugabe ni mgonjwa, amekuwa akifanya safari za Asia kupata matibabu.

Kadhalika Grace alinukuu kitabu cha 2Samuel: 9-1 kwamba “Kisha Daudi akasema, Je, amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya nyumba ya Jonathan.”

Grace ametoa kauli hiyo wakati makundi ya wanasiasa mashuhuri yakipigana vikumbo kutaka kumrithi Mugabe ambaye ameongoza nchi tangu uhuru.