Mke wa Waziri Mkuu awataka wanafunzi wa kike kujali muda

Muktasari:

Mke wa Waziri Mkuu amewakumbusha wanafunzi umuhimu wa kuutumia vizuri muda akisema kwamba wasipofanya hivyo watajuta baadaye kwa kuwa wakati ni mali na ukipita umepita.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa amewasihi wanafunzi wa kike nchini kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha kukatisha masomo yao.

Amesema ni vema wanafunzi hao wakatumia muda wao vizuri kwa kusoma kwa mfululizo kutoka kiwango kimoja cha taaluma kwenda kingine.

Mama Mary aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 23, 2017) alipozungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Vwawa, wilayani Mbozi.

Mke wa Waziri Mkuu ambaye ameambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ziara ya mkoani Songwe, aliwaasa wanafunzi hao kutumia wakati huu kwa kusoma kwa bidii na kujiepusha na vitendo viovu.

“Nawasihi mtumie muda huu kusoma kwa bidii ili muweke msingi imara kwa ajili ya kujenga maisha yenu ya baadae. Msikatishe masomo yenu,”amesema.

Ameongeza: “Utumieni muda huu vizuri ili msije mkaujutia baadaye, kwani wakati ni mali ukipita umepita.”

Amesema ni vizuri wakasoma hadi Chuo Kikuu na kwamba wasikimbilie kufanya mambo yasiyowahusu kwa sasa kwani mshika mawili moja lazima limponyoke.

Mke wa Waziri Mkuu amesema wanafunzi hao wakisoma hadi elimu ya juu watakuwa na uwezo wa kutambua jambo lipi ni jema na lipi ni baya.

“Kilichonifurahisha zaidi ni kwa sababu mimi pia ni mwalimu kwa hiyo ninavyoona wanafunzi wako vizuri kama hivi nafurahi sana, hivyo nawaomba msome kwa bidi,”amesema.

Serikali imetunga sheria kali dhidi ya watu wanaosababisha watoto wa kike kukatisha masomo yao kwa kuwapa mimba au kuwaoa.

Suala la wanafunzi kupata mimba na kuendelea na masomo limekuwa mjadala katika siku za karibuni baada ya Rais John Magufuli kusema kwamba Serikali yake haitosomesha wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shule.