Mkurugenzi Chadema ‘akwama’ polisi Dar

Muktasari:

  • Kigaila (pichani) anayetuhumiwa kutoa lugha ya uchochezi Oktoba 12 katika mkutano na waandishi wa habari alikutana na kadhia hiyo jana aliporipoti kituo kikuu cha polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemuweka rumande mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson.

Kigaila (pichani) anayetuhumiwa kutoa lugha ya uchochezi Oktoba 12 katika mkutano na waandishi wa habari alikutana na kadhia hiyo jana aliporipoti kituo kikuu cha polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Mwanasheria wa Kigaila, Frederick Kihwelo aliwaambia wanahabari nje ya kituo hicho kuwa hatima ya dhamana ya mkurugenzi huyo itaamuliwa leo.

“Amehojiwa kwa saa tatu kuanzia saa saba (mchana) hadi saa 10 (jioni) na amehojiwa kwa makosa aliyoyafanya katika mkutano wake wa Oktoba 12 na wamekataa kutoa dhamana labda hadi kesho (leo),’’ alisema.

“Lakini makosa yake yana dhamana ila wametueleza wanaoweza kuamua ama kupata dhamana au kukosa hawapo ofisini.”

Kihwelo alisema katika mkutano wa Kigaila na wandishi wa habari mkurugenzi huyo alizungumza mambo mengi ikiwamo kupigwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kutekwa kwa Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Kaimu kamanda wa kanda hiyo, Benedict Kitalika alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa upepelezi kwa sehemu kubwa umekamilika. “Upelelezi umekamilika, kilichobaki ni jalada lake kupelekwa kwa mwanasheria kazi ambayo itafanyika kesho (leo),” alisema Kitalika. “Tuombe uzima hiyo kesho (leo) tunalifanyia kazi kwa uharaka zaidi na hiyo kesho (leo) tutaona kama atapelekwa mahakamani au vinginevyo.”

Kigaila aliwasili kituoni hapo saa sita mchana akiwa ameongozana na mwanasheria wake, Kihwelo na mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casmil Mabina.