Mkurugenzi halmashauri Babati awashusha vyeo walimu wakuu 28, waratibu kata 10

Muktasari:

Halmashauri ya wilaya ya Babati ina shule za msingi 142 na ilishika nafasi ya tatu kati ya halmashauri saba za mkoa huo katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba wa mwaka jana.

Babati. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Hamis Malinga amewashusha vyeo walimu wakuu 28 wa shule za msingi na waratibu 10 wa elimu wa kata.

Amechukua uamuzi huo leo Januari 15, 2018  baada ya wanafunzi wa darasa la saba wa shule zao kutofikisha asilimia 50 ya ufaulu katika matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana. 

Halmashauri ya wilaya ya Babati ina shule za msingi 142 na ilishika nafasi ya tatu kati ya halmashauri saba za mkoa huo katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba wa mwaka jana. 

Malinga amesema walimu wakuu, waratibu elimu hao wamehusika kushuka huko kwa ufaulu kwa  maelezo kuwa wameshindwa kuwasimamia ipasavyo walimu wa shule zao. 

"Wanashindwa kusimamia elimu kwenye nafasi zao na hawachukui hatua yoyote ili kusaidia kwani mwalimu hafundishi, anachezacheza na mabinti shuleni, hawaandai maandalio ya masomo, tutaendeleaje kwa hivi?”amehoji Malinga. 

Amesema hali hiyo haikubaliki kwani walimu wakuu na waratibu hao hawachukui hatua wanaficha ukweli wakati wanatambua mwanafunzi asipofaulu ni kuharibu maisha yake ya baadaye. 

"Tunaweka mikakati na watendaji wanakuwa walimu wakuu na waratibu ila hawajali wanashindwa kusimamia wajibu wao tukaona watupishe waje wengine," amesema. 

Amesema japo wanapewa posho ya madaraka wanashindwa kusimamia elimu na mara nyingi wanapatiwa taarifa kuwa walimu wanafanya biashara hawafundishi  jambo ambalo linafichwa na  walimu wakuu na waratibu kila wanapoulizwa.

 "Tumeamua kutengua wadhifa wa walimu wakuu na waratibu elimu hao wa kata kutokana na ufaulu mdogo nawaomba madiwani kuwapa ushirikiano wa kutosha wateuzi wapya," amesema Malinga. 

Amesema watakaojaza nafasi hizo watateuliwa hivi karibuni ili washirikiane na walimu kuhakikisha wanafunzi wanasoma ipasavyo na kufaulu vizuri kwenye mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa mwaka 2018. 

Hata hivyo, mratibu wa mtandao wa asasi za kiraia mkoani Manyara (MACSNET), Nemency Iriya amepongeza hatua hiyo na kushauri utafiti mdogo ufanyike ili kubaini tatizo lililopo.