Mkurugenzi awaonywa wakandarasi Mbinga

Muktasari:

  • Mafita amesema Jumla ya Sh1 bilioni zimetolewa ikiwa ni bajeti ya kwanza kwa halmashauri hiyo mpya  kwa mwaka 2016 /2017 ambapo ukarabati wa barabara na ujenzi wa madaraja umeanza rasmi

Wakandarasi  ambao wamepewa tenda ya kujenga madaraja,  barabara na kufanya ukarabati za  Halmashauri ya Mji ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kufanya kazi  kwa kuzingatia  ubora na kuzikamilisha kulingana  na mikataba yao.

 Wito huo umetolea na Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Ismail Mafita wakati akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake.

Mafita amesema Jumla ya Sh1 bilioni zimetolewa ikiwa ni bajeti ya kwanza kwa halmashauri hiyo mpya  kwa mwaka 2016 /2017 ambapo ukarabati wa barabara na ujenzi wa madaraja umeanza rasmi .

Amesema halmashauri hiyo imeanza ujenzi wa madaraja pamoja na kukarabati barabara zake kwenye kata zote 19 zilizopo katika halmashauri hiyo ili kuondoa kero ambazo zilikuwa zikilalamikiwa na wananchi na hivyo kusaidia kurahisisha upatikanaji wa urahisi wa  huduma za jamii na ukusanyaji wa mapato .

Lakini amesema wananchi wataondokana na kero hizo ikiwa wakandarasi watafanya kazi kwa weledi na kukamilisha kwa wakati unaotakiwa kwa mujibu wa mikataba yao.

Mafita amesema ujenzi na ukarabati wa mindombinu hiyo umeanza tangu Mei 8, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.
Amesema jumla ya madaraja yaliyoanzwa kujengwa ni katika kata za Myangayanga , madaraja mawili Kata ya Luwahita, matatu Kata ya Mpepai moja Tulila, Kata ya Kihungu ambapo madaraja matatu yapo kwenye maandalizi.

Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ikiwa ni pamoja na kulinda mali na vifaa vya ujenzi vilivyopo katika maeneo yao ili kazi iweze kukamilika kwa wakati uliopangwa.