Mkutano Mkuu CCM Machi 12

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Humphrey Polepole

Muktasari:

Akizungumza kwenye kipindi cha Mada Moto kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Humphrey Polepole alisema mkutano umeitishwa kwa dharura kwa ajili ya kupitisha mabadiliko ya Katiba.

Dar es Salaam. Mkutano Mkuu wa CCM utakaopitisha mabadiliko ya katiba unatarajiwa kufanyika Machi 12.

Akizungumza kwenye kipindi cha Mada Moto kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Humphrey Polepole alisema mkutano umeitishwa kwa dharura kwa ajili ya kupitisha mabadiliko ya Katiba.

“Tunajua halmashauri kuu ina uwezo wa kupitisha mabadiliko halafu tukapeleka taarifa kwenye mkutano mkuu, lakini mwenyekiti (Rais John Magufuli) ameamua kuitisha mkutano wa dharura ili kupitisha mabadiliko hayo,” alisema Polepole na kuongeza: “Mabadiliko ambayo yanafanya mageuzi ndani ya chama.”

Polepole alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana Machi 10 na Halmashauri Kuu inaratajiwa kukutana siku inayofuata.

Pia, alisema tayari CCM imekubaliana na wenzao wa Chama cha Kikomunisti cha China kujenga Chuo Kikuu cha Chama, ambacho kitakuwa kinapika makada wake ili kuelewa itikadi yao.

 Kabla ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni (wakati huko Chuo cha Chama Kigamboni), ndicho kilikuwa kikiandaa makada hao.

Mwisho