Tuesday, February 13, 2018

Mkuu wa Mkoa azua kizaazaa

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane ili aweze kumpa msaada, lakini si diwani kutoka vyama vingine vya upinzani.

Kauli hiyo imewaibua wanasiasa na watu wengine wakisema ni kinyume cha utumishi wa umma.

Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara Kata ya Haydom wilayani Mbulu, Mnyeti aliwataka madiwani wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM ili waweze kushirikiana naye kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama tawala.

Hata hivyo, wanasiasa hasa wa vyama vya upinzani waliozungumza na Mwananchi jana wamesema kauli hiyo ni ya kibaguzi isiyofaa kuungwa mkono hata kidogo huku katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji akisema wanatafuta ushahidi ili walipeleke suala hilo mahakamani.

Mwananchi ilipomtafuta Mnyeti jana kutaka kujua nini maana ya kauli yake hiyo alisema, “Ni hivyo hivyo maana yake ni hiyohiyo. Kama ndio nimesema basi rudieni huwa sipendi kurudia maneno maana nimezungumza katika mkutano na umeshafanyika.

“Hivi tangu lini Chadema wakafanya kazi na CCM maana wao hawapendi ushirikiano. Labda nikuulize swali wewe mwandishi, unaweza habari ya Mwananchi ukaipeleka Majira?”

Kauli ya mkuu huyo wa mkoa katika mkutano wake pia ilizua mjadala mkali jana katika mitandao ya kijamii ya Mwananchi ya Instagram, Facebook na Twitter baada ya wasomaji kumkosoa kwa madai kauli aliyoitoa ni ya kibaguzi na haipaswi kutolewa na kiongozi.

Katika mkutano huo wa juzi, Mnyeti alisema ni vyema madiwani wa Chadema wakajiunga na CCM kwa sababu diwani wa Chadema ni ngumu kufanikisha maendeleo ya wananchi kwa madai kuwa hakuna ambaye atamsikiliza akiwasilisha hoja zake katika vikao vya halmashauri husika.

“Hata hapa Haydom najua ni ngome ya Chadema hata mwenyekiti wa kijiji namuona ana damu ya CCM, sasa ondokeni huko mje huku tutekeleze ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa kuleta maendeleo,” alisema Mnyeti.

Awali, mkazi wa Kata ya Hayderer, John Tluway aliuliza swali kwa mkuu huyo wa mkoa akitaka kujua sababu za Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga kutofika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema.

Akijibu swali hilo, Mnyeti alimpongeza Mofuga kwa kutokufika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema kwa maelezo kuwa diwani wa kata hiyo anapaswa kujiunga na CCM ili kufanikisha maendeleo.

“Mkuu wa wilaya ninakupongeza kwa wewe kutofika kwenye kata hiyo kwani ningepata taarifa umefika mara ya kwanza, mara ya pili na mara ya tatu ningekuwa na mashaka na wewe, lakini hongera sana kwa kutokwenda,” alisema Mnyeti.

Aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kutekeleza na kufanikisha kwa vitendo ilani ya CCM hata kama hawana kadi ya chama hicho kwani ndicho ambacho kipo madarakani.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbulu, Nasaeli Sulle alimhakikishia Mnyeti kuwa wananchi wa Haydom wamejitambua kuwa walifanya makosa kwa kuchagua Chadema ila sasa wapo tayari kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wakuu wa wilaya kupanda katika majukwaa ya kampeni za uchaguzi wa ubunge na kuwanadi wagombea wakitaka wachaguliwe, ili kurahisisha maendeleo katika maeneo husika.

Februari 22, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu alipanda jukwaani kumnadi mgombea wa CCM katika Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel kwenye viwanja vya KKKT Karansi na kusema Serikali haijaribiwi hivyo ni vyema kila mmoja akahakikisha anadumisha amani na kufanya siasa za kistaarabu katika kipindi chote cha kampeni

Alisema Dk Mollel ameleta heshima kwa wananchi wa Siha huku akiwataka wananchi wote kumuunga mkono na kuhakikisha anapata ushindi wa kishindo.

Pia, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando Februari 6, katika mkutano wa hadhara aliwatambulisha madiwani wa Chadema waliohamia CCM; Ayub Mlimba (Mwaka Kati), Simon Mbukwa (Kaloleni) na Amos Nzunda (Mpemba).

Mkuchika atoa neno

Alipoulizwa kuhusu viongozi wa Serikali kuwanadi wagombea majukwaani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika alisema viongozi hao wanatokana na uteuzi ndani ya CCM hivyo wanaruhusiwa kupanda jukwaani kama makada kupeperusha bendera ya chama chao.

“Wale ni wateule wa Chama cha Mapinduzi, wana haki ya kuwanadi wagombea wao kama chama ila hawaruhusiwi kuingia ndani kwenye utendaji wa kazi zao, wanatakiwa kunadi sera za chama na utekelezaji wa ilani. Kwa hiyo naweza kusema wanaruhusiwa na hakuna tatizo lolote,” alisema.

Wanasiasa

Katika maelezo yake, Dk Mashinji alisema, “Mnyeti ni kiongozi mkubwa katika Serikali, kauli yake ni ya kibaguzi na inakwenda kinyume na Katiba ya nchi yetu. Bado tunakusanya ushahidi ukikamilika tutamfikisha mahakamani ili akaeleze alikuwa na maana gani.”

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kauli ya Mnyeti inaweza ikasababisha fujo hivyo mamlaka yake ya uteuzi (Rais) inapaswa kulichukulia suala hilo kwa ukubwa wake.

“Rais kama anaitakia mema Serikali yake aangalie sana watendaji waliopo chini yake. Kauli ya Mnyeti ni ya kibaguzi na vyama vya kisiasa vipo kikatiba, lakini yeye hatambui,” alisema Mbatia.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga alisema, “Sisi Serikali tuliipa jukumu la kutekeleza ilani yetu kama kukiwa na changamoto tutaieleza.”

Maoni ya wasomaji

Katika mtandao wa kijamii wa facebook, mmoja wa wachangiaji, Mbaga Karim ameandika, “Duuuh viongozi wetu wamefikia hatua hii ya kutugawa kwa sababu ya itikadi za vyama vyetu?

“Kiongozi kama huyu anapaswa ajitathmini kwanza kama bado ana sifa ya kuwa kiongozi au imeondoka kwa kauli hiyo ya kibaguzi. Maendeleo hayaletwi na chama, bali yanaletwa na wananchi kwa ushirikiano tena kwa kuweka tofauti zetu za vyama pembeni. Kama tumefikia hapa hii ni hatari sasa.”

Mchangiaji mwingine, Zacharia Kayago alisema, “Cheo ni dhamana, hakuna atakayeishi milele..., wapo wengi waliokuwa na vyeo lakini leo tunakutana sokoni kununua mboga, hata sandles miguuni hana.

“... ipo siku hao Chadema ambao huwapendi unaowanyima haki zao za msingi kisheria na waliochaguliwa na wananchi utawaona wa maana. Mungu sikia kilio cha wengi, maana kilio cha wengi ni harusi! Ngoja nikae kimya.”

Naye Patano Kimath aliandika, “Mbona anajenga jamii katika matabaka? Ni vyema akamshauri mkuu kuvifuta vyama vya upinzani kuliko kuwanyanyasa wananchi kwa kigezo cha chama, huyu siyo wa kumnyamazia kabisa.”

“Viongozi wetu wanapaswa kupewa elimu juu ya uendeshaji wa Serikali chini ya mfumo wa vyama vingi. Nijuavyo baada ya uchaguzi, sote tunapaswa kushirikiana kuleta maendeleo. Chuki za nini?” amehoji Anko Matiku.

Kwa upande wake Sakhi Sisibo Tippe ameandika, “usema “Labda aseme tu hawezi kutoa msaada kwa wanachama wa Chadema sio diwani kwani msaada sio wa diwani ni wa wananchi.”


-->