Mkuu wa mkoa, mwenyekiti wa CCM wilaya walivyochuana

Muktasari:

  • Ngicho anadaiwa kuitisha mkutano na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho akiwataka wasitii agizo lililotolewa na Malima la kuwataka ndani ya siku 60 wawe wamehama eneo la hifadhi ambalo liliwekwa alama ya mpaka (bikoni) Aprili 14.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Ngicho mwishoni mwa wiki iliyopita aliingia katika mvutano na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alipogoma kuambatana naye kwenda Kijiji cha Nyanundu kukanusha kauli aliyoitoa kwa wananchi kuhusu mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Ngicho anadaiwa kuitisha mkutano na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho akiwataka wasitii agizo lililotolewa na Malima la kuwataka ndani ya siku 60 wawe wamehama eneo la hifadhi ambalo liliwekwa alama ya mpaka (bikoni) Aprili 14.

Video kuhusu majibizano kati yao ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzua mijadala kutoka kwa wananchi.

Hali ya kuwapo mvutano kati ya viongozi wa CCM na wa Serikali wanaotokana na chama hicho inaonekana kuongezeka baada ya Jumamosi, gazeti hili kuripoti mgogoro unaofukuta wilayani Mwanga ambako mkuu wa wilaya hiyo, Aaron Mbogho alidaiwa kumuweka mahabusu mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Jaffary Kandege.

Taarifa zinasema mwenyekiti huyo aliwekwa mahabusu Kituo cha Polisi Mwanga kabla ya kudhaminiwa na diwani wa Shighatini (CCM), Enea Mrutu.

Kandege alisema kwa hali ya mgogoro ilipofikia hayupo tayari kufanya kazi na Mbogho.

Lakini Mbogho alisema mwenyekiti huyo hakufikishwa polisi na kuhojiwa kwa wadhifa wake akitaka aulizwe aliandika maelezo kuhusu tuhuma gani.

Kuhusu mvutano kati ya Malima na Ngicho, mazungumzo kati yao kwenye video iliyosambaa ni kama ifuatavyo:

Malima: Twende sasa hivi.

Ngicho: Aah! Nyanundu siendi.

Malima: Aah! Huwezi kusema hivyo mimi ndiye ninayekwambia tutakwenda. Haki ya Mungu nakwambia.

Ngicho: Samahani mkuu naumwa sana, naumwa sana, naumwa, naharisha, naharisha.

Malima: Nakuhakikishia mwenyekiti. Potelea mbali mwenyekiti tunabeba na maji mtoni, twende ukawaambie wale wananchi kuwa Serikali nchi hii ni moja basi.

Ngicho: Hapana, hapana, hapana. Naomba umchukue na Heche umwambie, hivyo maana mimi ni kiongozi wa chama.

Malima: Nasema hivi, wewe uliitisha mkutanao kule kwa hiyo leo tutakwenda Nyanundu.

Ngicho: Sijaitisha mkutano mkuu, mimi nilikuta watu wamejaa pale wakanizuia.

Malima: Basi watakukuta leo, twende hata wakitukuta watu wawili.

Ngicho: Hapana kiongozi.

Alipoulizwa kuhusu video hiyo, Malima alisema alimtaka mwenyekiti huyo kuongozana naye kwenda kijijini kutatua mgogoro uliopo baina ya Serikali na wananchi kuhusu uwekaji wa mipaka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Kiongozi huyo wa chama alifanya mkutano katika Kijiji cha Nyanundu ambacho kipo ndani ya hifadhi na kuwataka wananchi wakaidi agizo nililotoa siku chache kabla ya mkutano wake nikiwataka walio ndani ya bikoni waondoke ndani ya siku 60 naye alikuwa akikataa,” alisema Malima.

Alisema alikuwa akitaka mwenyekiti huyo akakanushe kauli aliyoitoa kwa wananchi kuwa wasiondoke eneo hilo.

“Serikali ina sheria na sheria hizo hazina kushoto wala kulia, ukiambiwa na Serikali usifanye hiki acha. Sasa unapokaidi agizo lazima uchukuliwe hatua. Yule mwenyekiti alikwenda mwenyewe kwenye hicho kijiji na kuwataka wananchi wakiuke agizo la Serikali,” alisema.

Kwa upande wake, Ngicho alisema Malima alimfuata nyumbani kwake Kijiji cha Kariyashanga na kumlazimisha aende kuwaambia wananchi wa Nyanundu wahame naye alikataa.

“Ni kweli nilikataa na hiyo kuharisha nilisema tu kama sehemu ya kujitetea lakini ukweli ni kwamba, Serikali lazima isikilize chama kinasema nini isifanye tu hata kama inawaumiza wananchi,” alisema Ngicho.

Alisema yeye ni kiongozi wa chama na ni mwanasiasa. Ngicho alisema alikwenda katika kijiji hicho na kamati ya siasa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walikuwa wakilia na kuimba, ‘CCM inatutesa inatunyang’anya ardhi’.

“Tulipata taarifa kwamba wananchi zaidi ya 42 wamekamatwa na wamepigwa. Nilipata taarifa hizo nikiwa Dar es Salaam, nikampigia simu DC wa Tarime twende tukatembelee hayo maeneo akaniambia yuko Simiyu ikabidi tuondoke na kamati ya siasa,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema walipofika aliwakuta wananchi wenye hasira waliowazingira na kuwataka wazungumze chochote hivyo iliwalazimu kuwatuliza kwa kuwaeleza kuwa wakae watulie na wasubiri kauli ya naibu waziri mwenye dhamana ambaye atakwenda kuwasikiliza.

“Kwa kuwa ni mwanasiasa niliwaambia wananchi wawe wavumilivu naibu waziri anakuja. Viongozi wa Serikali waliposikia, kina Malima likawaudhi. DC akaja kwangu hakunikuta, siku ya pili akanikuta ndipo Malima akaanza kunilazimisha niende nikawaeleze wale wananchi kuwa ile mipaka ni halali na wananchi waiheshimu,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema, “Niliona suala la kwenda kutamka hivyo litaniumiza kisiasa, nikakataa. Alinilazimisha twende kule jambo ambalo haliwezekani kwangu kwa kuwa kufanya hivyo ni kukidhalilisha chama changu.”

Ngicho alisema hawezi kwenda katika kijiji hicho kuwaeleza wananchi wahame eneo hilo kwa kuwa wamekaa hapo muda mrefu na uwekaji wa bikoni haujawashirikisha.

“Mimi mwenyewe nimejenga, nina hoteli iko ndani ya bikoni lakini kuwa ndani ya bikoni hakunizuii kuwatetea wananchi,” alisema.