Mlinzi TanzaniteOne aua mwanakijiji

Muktasari:

Tibishubwamu amesema tukio hilo limetokea juzi kwenye eneo la kampuni hiyo ambapo mkazi wa Kijiji cha Naisinyai Kadogo Joseph (17) amepigwa risasi ya kichwa iliyosababisha kifo chake.

Mirerani. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Longinus Tibishubwamu amesema mtu mmoja amepigwa risasi na mlinzi wa kampuni ya TanzaniteOne.

Tibishubwamu amesema tukio hilo limetokea juzi kwenye eneo la kampuni hiyo ambapo mkazi wa Kijiji cha Naisinyai Kadogo Joseph (17) amepigwa risasi ya kichwa iliyosababisha kifo chake.

Kamanda huyo amesema chanzo cha mlinzi huyo kufanya hivyo ni wakati akiwafukuza wezi wasiibe vyuma chakavu katika eneo la kampuni hiyo.Amesema mlinzi huyo alitumia silaha aina ya shortgun mali ya kampuni ya TanzaniteOne.

“Mlinzi huyo alimjeruhi kwa kumpiga risasi sehemu ya kichwani ndipo akapelekwa hospitali ya Seliani iliyopo jijini Arusha, lakini alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu,” amesema kamanda huyo.

Ameongeza kuwa silaha, risasi tatu na maganda mawili vimehifadhiwa polisi kwa hatua zaidi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai, Taiko Kuriani amesema tukio hilo ni geni kwenye eneo hilo kwa kuwa hakuna mtu aliyewahi kupigwa risasi na kampuni hiyo, hivyo wameshangazwa na jambo hilo la mwana kijiji kuuawa.

Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Halfan Hayeshi amesema wamekutana na viongozi na jamii wa eneo hilo ili kuwekana  sawa.

“Kampuni itabeba jukumu la kufanikisha mazishi hayo na tunasubiri taarifa ya askari ambao bado wanaendelea na uchunguzi wa mauaji hayo ili watoe taarifa kamili juu ya tukio hilo,” amesema Hayeshi.