Mmoja afariki basi likinusurika kuingia Ziwa Victoria

Muktasari:

Dereva wa basi hilo, Idd Omary alijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali ya misheni Bukumbi kwa ajili ya matibabu.

 


Mwanza. Mtu mmoja amefariki na wengine  zaidi ya 30 wakiponea chupuchupu kuzama Ziwa Victoria, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kufeli breki.

Hata hivyo, dereva wa basi hilo la Kampuni ya Sabco alifanikiwa kulielekeza basi hilo kwenye ukuta wa ofisi za Kivuko cha Kigongo-Busisi, wilayani Misungwi.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Mkadam Mkadam amesema ajali hiyo imetokea saa saba na robo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 31 kujeruhiwa kati yao 10 walihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando. 

Dereva wa basi hilo, Idd Omary alijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali ya misheni Bukumbi kwa ajili ya matibabu.

Kamanda  Mkadam ametaja chanzo cha ajali hiyo ni basi hilo kufeli breki na hivyo dereva akalazimika kulibamiza kwenye ukuta wa ofisi ya Temesa. 

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Misheni Bukumbi,  Deusdedith Baluhya amesema amepokea majeruhi 32  na mmoja amefariki dunia.  

Amesema kati ya majeruhi hao, wapo watoto wanne wenye umri wa chini ya miaka mitano, kati yao wakike  ni watatu na wakiume mmoja.