Mnada wapaisha bei ya korosho hadi Sh3,670

Korosho ghafi zikiwa kwenye hatua ya kwanza baada ya kuchumwa kutoka shambani. Picha ya Mtandao

Muktasari:

  • Mnada wa kwanza wa wazi ulifanyika juzi katika ghala la Chama cha Msingi cha ushirika Muungamo lililopo kijiji cha Namyomyo wilayani Masasi.

Mtwara. Kwa mara ya kwanza wakulima wa korosho mkoani hapa, wameuza zao hilo kwa mnada na kupata bei kubwa ya Sh3,670 kwa kilo moja ya korosho ghafi badala ya Sh2,400 za msimu uliopita.

Mnada wa kwanza wa wazi ulifanyika juzi katika ghala la Chama cha Msingi cha ushirika Muungamo lililopo kijiji cha Namyomyo wilayani Masasi.

Katika mnada huo, wakulima walishuhudia bei zikishindanishwa kampuni 27 zilizoomba kununua korosho, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kutaka wakulima kushirikishwa katika mnada.

Meneja mkuu wa Chama kikuu cha Masasi-Mtwara (Mamcu), Kelvin Rajabu alisema waliamua kufanyia mnada kijijini hapo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kutaka wakulima wa korosho washirikishwe katika minada.

Rajabu alisema barua za kuomba zabuni ya kununua korosho zilikuwa za siri, zilisomwa mbele ya wakulima na mwisho walichagua kampuni iliyotangaza bei kubwa kuliko.

“Tumetekeleza agizo la Serikali la kufungua minada katika wilaya, wakulima wameshiriki na kufanya maamuzi, kwa maana hiyo utaratibu huu ni mzuri kwani unatoa fursa kwa wananchi na viongozi kuona na kushiriki moja kwa moja.

“Hili kwetu sisi kama chama kikuu ni faraja kwa sababu wakulima wenyewe ndiyo wamefanya maamuzi moja kwa moja na sisi tutaendelea kuwafuata walipo,” alisema Rajabu.

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe alisema kufanyika kwa mnada huo mbele ya wakulima na viongozi utasaidia kuondoa malalamiko yaliyokuwapo na sasa wakulima watakuwa wakiamua wenyewe bei ambayo itaweza kusaidia kuendana na gharama za uzalishaji na kuwataka kupeleka korosho zao kwenye maghala kwa wakati. “Tumeshuhudia mnada mpaka mwisho na wakulima wameamua wenyewe bei, mimi niwashauri wakulima kwa kipindi hiki ambacho korosho inahitajika sana wazipeleke maghalani kwa wakati ili waweze kupata bei nzuri.

“Hii itamsaidia sana mkulima hasa akishuhudia mwenyewe mnada, kwani tulikuwa tukisikia malalamiko mengi kwamba kuna wizi na bei zinapangwa, lakini leo wameshiriki wenyewe ingawa bado tunahitaji kuboresha zaidi ili mkulima aweze kunufaika zaidi,” alisema Mwambe.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Selemani Mzee alizitaka kampuni zilizoshinda zabuni ya kununua mazao hayo kulipa fedha hizo ndani ya siku sita na kupunguza korosho kwenye maghala makuu ili kupata nafasi kwa ajili ya shehena nyingine.

“Wakulima kero yao kubwa ni kucheleweshewa malipo mlionunua leo hakikisheni ndani ya siku sita mmepeleka pesa benki kulipa na baada ya hapo punguzeni mizigo kwenye maghala ili mizigo mingine iweze kuingia, atakayeshindwa kutekeleza masharti atachukuliwa hatua,” alisema Mzee.

Akizungumza hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini (CBT), Mudhihir Mudhihir alisema kampuni 66 zilichukua leseni ya kununua korosho ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka kampuni 54 kwa msimu uliopita na kuwa minada itakuwa ikifanyika kila wiki kutegemea korosho zitakavyokusanywa kutoka kwa wakulima kwenda maghalani.