Mnangagwa ataka kuhakikishiwa usalama

Muktasari:

Mnangawa, ambaye amedokeza kwamba hatarejea Zimbabwe hadi ahakikishiwe usalama wake, alisema mzozo uliopo sasa nchini humo unawahusu watu wa Zimbabwe na Mugabe.

Cape Town, Afrika Kusini. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa aliyeko uhamishoni amemwambia Rais Robert Mugabe kwamba mzozo wa sasa wa kisiasa na kikatiba nchini hauwahusu wawo wawili tu.

Mnangawa, ambaye amedokeza kwamba hatarejea Zimbabwe hadi ahakikishiwe usalama wake, alisema mzozo uliopo sasa nchini humo unawahusu watu wa Zimbabwe na Mugabe.

"Wananchi wa Zimbabwe wamezungumza kwa uwazi juu ya suala hili. Kwangu mimi sauti ya watu ni sauti ya Mungu na wao wamejieleza vizuri kuhusu kukosa kwao imani na uongozi wa Rais Mugabe. Vikundi kadhaa vya watu wakiwemo wanafunzi, wafanyakazi, wapinzani, wafanyabiashara ndogondogo, taasisi za kidini na raia wa kawaida wakiongozwa na maveterani, wajumbe wa chama chetu cha Zanu-PF, asasi za kiraia na watu wa rangi zote na imani tofauti nchini Zimbabwe wameonyesha kwa maandamano yasiyo na vurugu shauku yao kutaka Mheshimiwa Komredi Robert Gabriel Mugabe ajiuzulu," amesema Mnangagwa.

"Ni wito wangu kwa Rais Mugabe kwamba sasa aisikie sauti ya juu ya watu wa Zimbabwe inayomtaka ajiuzulu ili nchi iweze kusonga mbele na kulinda heshima yake iliyotukuka," amesema Mnangagwa.

Taarifa ya Mnangagwa imekuja wakati mkuu wa jeshi Jenerali Constantino Chiwenga amesema kwamba mchakato umekamilika juu ya mazungumzo kufikia mpango juu ya kuondoka kwa Mugabe.

Vilevile Chiwenga amesema Mugabe anafanya mawasiliano na Mnangagwa.