Sunday, January 14, 2018

Mnyeti awajia juu wanasiasa wanaochochea migogoro

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi jlyimo@mwananchi.co.tz

Kiteto. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewapa onyo wanasiasa wilayani hapa akisema atawachukulia hatua pindi watakapochochea na kusababisha migogoro ya ardhi kwa wananchi.

Akizungumza juzi kwenye kata ya Njoro, Mnyeti alisema atawachukulia hatua wanasiasa hao akitahadharisha kwamba yeye si mkuu wa mkoa wa maboksi anayeogopa kulowanishwa na mvua.

Alisema alipata taarifa ya baadhi ya wanasiasa wanaotumia migogoro ya ardhi kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa, hivyo hatawafumbia macho.

“Tumekuwa na migogoro isiyokwisha, wewe una shamba lako kwenye Kijiji cha Bwawani, kuna mtu anakuzuia kulima hapa Njoro? Au ukiishi hapa Njoro kuna mtu amekunyima kununua nyumba kule Kibaya makao makuu ya wilaya?” Alihoji Mnyeti.

Alisema atawashughulikia wanasiasa hao wanaochochea migogoro ya ardhi baina ya watu na watu na kijiji na kijiji ili iwe funzo kwa wengine.

Hata hivyo, alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhandisi Tumaini Magessa kuhakikisha vijiji vyote vinawekewa alama za mipaka ili kuondokana na migogoro ya ardhi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Lairumbe Mollel ambaye pia ndiye Diwani wa Chapakazi ni mmoja kati ya viongozi wanaotajwa kusababisha migogoro hiyo wilayani Kiteto ila alikana kujihusisha nayo.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa afanye uchunguzi wake na atabaini kuwa mimi sihusiki na uchochezi wa migogoro hiyo ya ardhi zaidi ya kuongoza halmashauri yangu ya wilaya kupitia nafasi hii,” alisema Mollel.

Mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian ambaye naye anatajwa kuhusika na uchochezi wa migogoro alisema wapinzani wake wa kisiasa ndiyo wanaosambaza habari hizo potofu kwani yeye hahusiki.

Awali, mmoja kati ya wakazi wa Njoro, Amina Omary alisema wanasiasa hao wamekuwa mwiba kwa kuchonganisha wakulima na wafugaji kwa lengo la kujipatia kura mara kipindi cha uchaguzi kitakapofika.

-->