Mnyika: Viongozi ondoeni woga, simamieni haki

Muktasari:

  • Mnyika aliyasema hayo kwenye kikao cha viongozi cha mashauriano kilichofanyika mkoani hapa juzi.

Shinyanga. Naibu katibu mkuu Chadema Bara, John Mnyika amewataka viongozi wa chama hicho mkoani Shinyanga kuishi bila hofu na waendelee kusimamia maendeleo na haki za wananchi.

Mnyika aliyasema hayo kwenye kikao cha viongozi cha mashauriano kilichofanyika mkoani hapa juzi.

“Kuna watu wanatishwa, wanabambikiziwa kesi na kushambuliwa hali ambayo inawafanya viongozi kuwa na hofu na kushindwa kukemea ufisadi,” alisema Mnyika na kuongeza: “Nawasihi viongozi wenzangu tusikubali kutiwa hofu, kwa kuwa tukikubali tutawahalalisha kubaki madarakani.”

Alisema Serikali imeshindwa kutatua kero za msingi za wananchi, kwani imetenga kiwango kidogo cha fedha kwenye mahitaji ya msingi ya wananchi.

Mnyika alisema kutokana na hali hiyo, Rais anapaswa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake kuwa amepambana na ufisadi, ilhali wananchi wanateseka na maisha.

Naye katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Renatus Nzemo alisema Serikali inajinadi kukusanya fedha nyingi, lakini kwa wananchi hazionekani.

Nzemo alisema licha ya sekta ya afya kutengewa fedha nyingi, hospitali nyingi hazina dawa za kutosha na wagonjwa wanaelekezwa wakanunue madukani.

Akizungumza kwenye mkutano huo, makamu mwenyekiti Kanda ya Serengeti, Gimbi Masaba ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu aliwataka viongozi hao wazingatie maadili na kuendelea kukijenga chama ili kiendelee kusimamia vizuri miradi ya wananchi wake.