Moi yaamriwa kulipa fidia ya Sh100 milioni

Emmanuel Didas akiwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere wakati alipokuwa akipelekwa India kwa matibabu mwaka 2007. Picha ya Mtandao

Muktasari:

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri hiyo baada ya Didas kushinda kesi ya madai aliyoifungua dhidi ya taasisi hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (wakati huo) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

 Mahakama Kuu imeamuru Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), kumlipa fidia ya Sh100 milioni Emmanuel Didas aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu kutokana na madhara aliyoyapa kimwili na kiufahamu.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri hiyo baada ya Didas kushinda kesi ya madai aliyoifungua dhidi ya taasisi hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (wakati huo) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Didas alifanyiwa upasuaji usio sahihi wa kichwa badala ya mguu ambao ulikuwa na tatizo mwaka 2007.

Akitoa mchanganuo wa fidia katika hukumu ambayo Mwananchi imeiona nakala yake, Jaji Zainabu Muruke alisema Sh1,076,620 ni fidia maalumu kwa kukosa kipato kwa kipindi cha miezi 21.

Huo ni muda ambao Didas alikaa hospitalini tangu Novemba Mosi, 2007 alipofanyiwa upasuaji hadi Agosti 24, 2009 alipoajiriwa na Moi kama mhudumu wa karakana.

Jaji Muruke alisema kipindi kabla ya kuajiriwa na Moi, Didas ambaye ni fundi pikipiki kulingana na ushahidi wake, alikuwa akijipatia kati ya Sh15,000 na Sh25,000 kwa siku.

“Anastahili fidia ya hasara maalumu kwa mapato aliyoyakosa kwa miezi 21,” anasema Jaji Muruke katika hukumu.

Alisema katika kukokotoa fidia aliyostahili, alitumia waraka wa Serikali namba 2 wa mwaka 2007 kuhusu kima cha chini cha mshahara.

Katika hukumu iliyotolewa na mahakama wiki iliyopita kwa matumizi rasmi, Jaji Muruke amebainisha Sh10.6 milioni ni gharama za huduma za nyumbani.

Amesema kiasi hicho ni fidia ya miaka 40 (wakati akiruhusiwa kutoka hospitalini), muda ambao alikuwa amebakiza kufikia umri wa kustaafu kwa lazima ambao ni miaka 60.

Jaji alisema kwa mujibu wa ushahidi wa Didas ambao haukupingwa na wadaiwa, kutokana na madhara aliyoyapata, ni mtu ambaye anahitaji msaada kwa watu wengine kwa maisha yake yote akiwa nyumbani.

Alisema Sh88,323,380 ni fidia ya maumivu na mateso aliyoyapata kutokana na upasuaji usio sahihi uliotokana na uzembe wa wataalamu katika kumhudumia.

Jaji Muruke alisema ametafakari namna tukio hilo lilivyotokea na kujiridhisha kuwa ni ajali isiyokusudiwa, pamoja na utayari wa mdaiwa (Moi) kumwajiri Didas kama sehemu ya uponyaji na kipato kwa njia ya mshahara.

Alisema amezingatia kuwa mdai anaishi katika hali ya kutokujiweza katika maisha yake yote yaliyosalia, huku akikosa kufurahia huduma muhimu ambazo angeweza kuzipata ikiwamo kuoa, kama alivyodai mahakamani kuwa kwa hali aliyo nayo, wasichana wamekuwa wakimkataa.

Alisema licha ya madhara aliyoyapata ikiwa ni pamoja na kupooza upande mmoja wa mwili na matatizo ya kiufahamu, hakuna kiwango chochote cha fidia kinachoweza kumrejesha katika hali yake ya awali.

“Mdai anastahili fidia kwa maumivu na mateso. Kwa kuzingatia hayo ninampa Sh88,323,380 kwa maumivu na mateso,” anasema Jaji Muruke katika hukumu hiyo.

Jaji Muruke ameiamuru Moi kumlipa Didas riba ya asilimia saba kwa fidia ya hasara ya kukosa kipato kwa miezi 21 na kwa fidia ya maumivu na mateso yaliyotokana na makosa hayo, kutoka siku ya hukumu hadi malipo yote yatakapokamilika.

Pia, alisema iwapo Moi itakatisha mkataba wa ajira kwa sababu zozote zile, italazimika kumlipa mshahara na mafao mengine kwa muda wote atakaokuwa amebakiza kustaafu kwa lazima.

Wakili Cornelius Kariwa aliyemwakilisha Didas katika shauri hilo alisema kuwa Moi imewapatia taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyotolewa Agosti 30, mwaka jana.

Msemaji wa Moi, Almas Jumaa alipoulizwa kuhusu hukumu hiyo alisema hana taarifa kwa kuwa shauri hilo lilishughulikiwa na Wizara ya Afya.

Kesi hiyo namba 129 ya mwaka 2012, ilifunguliwa na Sisti Marishay kwa niaba ya Didas kutokana na hali yake ya kupooza.

Didas alifanyiwa upasuaji wa kichwa alipofikishwa hospitalini Moi kutokana na ajali aliyoipata na kuumia mguu. Wakati akifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu, mgonjwa mwenzake aliyekuwa amelazwa hapo, Emmanuel Mgaya alifanyiwa upasuaji wa mguu ambao haukuwa na tatizo badala ya kichwa.

Kutokana na makosa hayo, wagonjwa wote wawili walipelekwa katika hospitali ya Indraprastha Apollo, nchini India kwa matibabu zaidi. Mgaya alifariki dunia baadaye.