Mpambano mkali JPM vs Chadema

Rai John Magufuli akihutubia wakazi wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida baada ya kuwasili wilayani hapo akiwa njiani kwenda Singida mjini jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

Mikutano na maandamano hayo ni sehemu ya operesheni ya Chadema kupinga kile inachokiita kuwa ni ukandamizaji wa demokrasia, ikiwa imepewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akisisitiza tamko lake la kuzuia shughuli za kisiasa kwa wagombea walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, Chadema imetia mkazo katika uamuzi wake wa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi.

Mikutano na maandamano hayo ni sehemu ya operesheni ya Chadema kupinga kile inachokiita kuwa ni ukandamizaji wa demokrasia, ikiwa imepewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).

Rais Magufuli alikuwa mkoani Singida jana ambako alieleza msimamo wake kuwa amezuia mikutano ya kisiasa kwa wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, akitahadharisha kuwa asijaribiwe.

Lakini, jijini Dar es Salaam, viongozi wa Chadema walikutana na waandishi wa habari na kuelezea jinsi wabunge wao wanavyozuiwa kufanya mikutano na wananchi, huku wakinukuu vipengele kadhaa vya Sheria ya Vyama vya Siasa, kanuni na Katiba vinavyotoa haki ya kufanya mikutano ya kisiasa bila ya kusubiri kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

CCM nayo ilitoa kauli juzi, sambamba na Msajili wa Vyama vya Siasa, ikielezea uamuzi wa Chadema kuwa ni wa uchochezi.

“Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma,” alisema Rais Magufuli mkoani Singida ambako alihutubia wananchi wakati akiwa njiani kuelekea Kahama.

“Wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia, wakawaeleze vizuri. Mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa.

“Wananchi hawa wana shida. Siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa.”

Rais alifafanua kuwa alichozuia ni watu kutoka kwenye eneo lao na kwenda kushawishi watu waandamane kwenye eneo jingine, huku akitoa mfano unaoonekana kumpiga kijembe mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

“Siyo mtu anatoka Hai kwenda Kahama kushawishi watu wafanye fujo,” alisema Rais akionekana kurejea kitendo cha Mbowe, ambaye ni mbunge wa Hai, kwenda Kahama ambako chama chake kilisema kingetumia mkutano wa hadhara kumshtaki Rais kwa wananchi.

Jijini Dar es Salaam, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari kuwa utekelezaji wa mikakati mitatu ya chama hicho kupinga kile inachokiita kuwa ni ukandamizaji wa haki na demokrasia unaofanywa na Serikali, uko palepale.

Alisema mashirika, taasisi na watu wa kada mbalimbali wameonyesha nia ya kushirikiana nao “kudai demokrasia”.

“Hatutarudi nyuma,” alisema Mwalimu kwenye mkutano na waandishi wa habari.

“Mkakati wetu wa Septemba Mosi uko pakepale. Tumetiwa moyo na watu mbalimbali ambao nao wanakerwa na mambo yanayofanywa na Serikali. Tunazungumza nao na tutashirikiana nao. Tunachokidai ni haki yetu na tutaendelea na operesheni Ukuta.”

Katika mkutano huo, chama hicho kimemjibu Jaji Francis Mutungi kwamba si kweli kuwa Chadema inakiuka Sheria Namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 9 (2) (c), huku ikinukuu vifungu vya sheria hiyo na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za mwaka 2007, zinazotoa haki kwa chama cha siasa kufanya mikutano na maandamano.

Kauli hiyo ya jana ya Chadema ililenga kumjibu Jaji Mutungi na msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, ambao juzi walikituhumu chama hicho kutoa kauli walizodai zimejaa uchochezi.

Mlezi huyo wa vyama vya siasa na Ole Sendeka walikuwa wakijibu maazimo ya Kamati Kuu ya Chadema yaliyosomwa siku tatu zilizopita na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambayo yaliweka mikakati hiyo inayoashiria kupinga kauli ya Rais kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Chama hicho pia kimeanzisha operesheni Ukuta, ikitaja mambo 11 inayodai kuwa ya ukandamizaji wa demokrasia na mengine 24 yaliyosababisha kuzinduliwa operesheni hiyo.

Jeshi la Polisi lilivunja mkutano wa hadhara wa Chadema uliopangwa kufanyika Kahama kwa madai kuwa ulilenga kushawishi wananchi wasitii maagizo ya Serikali na baadaye kutangaza kuzuia mikutano yote ya hadhara na maandamano.

Siku chache baadaye, Rais Magufuli alitangaza kuzuia shughuli za kisiasa hadi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020 akisema wakati wa siasa ulishaisha na uchaguzi, na kusisitiza kuwa asingependa “kuona mtu yeyote akimchelewesha kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi”.

Pamoja na Jaji Mutungi kujaribu kufafanua kuwa tamko hilo halikumaanisha kupiga marufuku shughuli za siasa, Rais Magufuli alisisitiza kauli yake kwenye hafla ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kuwa asingependa kuona akicheleweshwa kutekeleza ahadi zake na kutaka chombo hicho cha dola kutekeleza agizo hilo.

Jeshi la Polisi pia lilizuia mkutano wa ndani wa chama cha ACT Wazalendo uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili bajeti ya Serikali ya 2016/17.

Mvutano

Katika ufafanuzi wake Mwalimu alisema mkutano wa jana na waandishi wa habari ulilenga kueleza msimamo wa chama hicho kuendelea na mipango yake ya kufanya maandamano na mikutano nchi nzima, sambamba na kushirikiana na watu mbalimbali, huku akieleza Jaji Mutungi anavyoshindwa kufanya kazi yake ya kuvilea vyama vya siasa.

“Msajili ameshajiondolea uhalali wa kutusimamia na kutukosoa. Rais amepiga marufuku mikutano ya siasa, mbona Jaji Mutungi hakuviita vyama tukazungumza kauli hii ya Rais? Iweje chama kizuiwe kufanya shughuli za siasa kinyume na sheria na kanuni na yeye anakaa kimya wakati ushahidi anao?” alihoji.

Mwalimu alitoa mfano jinsi viongozi wa Chadema walivyozuiwa kuingia kwenye ofisi za chama hicho Juni 8 mjini Shinyanga kutia saini kitabu cha wageni baada ya Jeshi la Polisi kuzuia shughuli yoyote ya chama cha siasa mjini humo, ikiwa ni siku moja baada ya kuzuia mkutano wa hadhara wa chama hicho, mjini Kahama.

“Wabunge wetu wawili wa Arusha na wenyeviti wawili wa halmashauri wameitwa polisi kujieleza sababu za kufanya mkutano wa hadhara. Wabunge wetu wanazuiwa kufanya mikutano ya hadhara. Mikutano ya chama tunaomba vibali na kunyimwa. Haya yote Msajili hajayaona?” alihoji Mwalimu.

Alihoji ni taratibu na sheria zipi ambazo Jaji Mutungi anavitaka vyama vya siasa kuzingatia kabla ya kufanya mikutano zaidi ya kutoa taarifa polisi. Alisema Chadema wanazingatia taratibu hizo, lakini hawaruhusiwi.

“Aseme hatujazingatia nini. Tuna barua nchi nzima za kuomba mikutano na polisi wamezuia. Sasa yeye anataka tukae kimya tu na tusifanye shughuli za siasa? (Jaji Mutungi) Anashindwa hata kuikemea Serikali kwa yanayotokea Zanzibar?” alihoji.

Juzi katika tamko la CCM, Ole Sendeka alisema Serikali haijazuia mikutano ya wabunge kwenye majimbo yao.

“Wabunge wako huru kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao na tumeona wakifanya, wakiwemo wa vyama vya upinzani. Pia vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama vyao haijazuiwa, ndiyo maana vyama vinafanya mikutano yake ya kikatiba bila tabu,” alisema Ole Sendeka.

Kuhusu lugha za matusi na uchochezi ambazo chama kinadaiwa kuzieneza, Mwalimu alisema anashanga kuona Jaji Mutungi akikaa kimya wakati katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, viongozi wa chama hicho tawala walimtukana na kutoa lugha za uchochezi dhidi ya aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa.

“Msajili anasema tamko letu la mikutano nchi nzima limejaa uchochezi. Leo tutatuma watendaji wa chama kumpelekea tamko hilo ofisini kwake alisome, atueleze uchochezi wetu uko wapi,” alisema Mwalimu.

Mvutano wa kanuni

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kauli ya Jaji Mutungi kwamba Chadema imekiuka kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za mwaka 2007 si ya kweli.

Mrema alivitaja vifungu vya 4(1) (e) na 5(1) (c) (i) vya kanuni hiyo, kusisitiza kuwa vinatoa haki kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake, kuzuia chama tawala kuvuruga shughuli za siasa za vyama vingine kwa kutumia dola.

Alisema kifungu cha 4(1) (e) kinasema; kila chama cha siasa kitakuwa na haki za kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, wakati kifungu cha 5(1) (c) kinaeleza wajibu wa vyama kutotumia vyombo vya dola kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama cha siasa kingine kwa manufaa yake.

Kifungu hicho pia kinataka vyama kuepuka kutumia mamlaka, rasilimali za Serikali, vyombo vya dola, na wadhifa wa kiserikali, kisiasa au ufadhili wa nje ama wa ndani kwa namna yoyote ile ili kukandamiza chama kingine.

“Msajili ni Jaji, sisi (Chadema) tulijua kuwa atakuwa tofauti, lakini amekuwa kama mtangulizi wake. Tunamtaka afuate sheria na kanuni ambazo Lowassa alizisaini alipokuwa Waziri Mkuu. Kwa sasa yupo Chadema anazijua vizuri hizo kanuni na utekelezaji wake na hazina shida zipo wazi tu,” alisema Mrema.

Katika maelezo yake ya juzi, Jaji Mutungi alisema tamko la Chadema kuhusu maandamano na mikutano ya hadhara limejaa lugha za uchochezi, kashfa na kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Huku akinukuu vifungu vya kanuni hiyo, Jaji Mutungi alisema kifungu 9(2)(f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Kanuni ya 5(1)(d) inakitaka kila chama cha siasa kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni uongo. Kuhusu mtu yoyote au chama cha siasa. Tamko la Chadema ni ukiukwaji wa sheria na si mara ya kwanza chama hiki kutoa kauli hizi,” alisema Jaji Mutungi.