Samia ataka mpango wa kuiboresha Dar

Muktasari:

Mpango huo mmoja wa kuboresha mazingira ili kujikinga na maafa yatakayotokana na mvua hasa mafuriko

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu amewataka viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia ngazi za wilaya, halmashauri kuwa na mpango mmoja wa kuboresha mazingira ili kujikinga na maafa yatakayotokana na mvua hasa mafuriko.

Mama Samia amesema hayo leo Ijumaa wakati akifungua mkutano unaokutanisha wadau wa mazingira wa jiji hili ambao una lengo la kuja na mpango kazi wa kuondoa majanga hasa mafuriko.

Mkutano huo ambao umeudhuriwa na viongozi na mawaziri mbalimbali akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na wakuu wa wilaya.

Samia amesema katika maafa yanayotokea katika jiji la Dar es Salaam kumekuwa na mipango tofauti katika wilaya zote jambo ambalo sio sawa kwani lazima kuwe na mkakati wa kunusuru jiji zima.

"Lazima tuwe na mkakati kabambe wa kufanya usafi wa mifereji na hatuwezi kusubiri maafa ndio tuanze kufanya kazi ya uokoaji sio sawa kabisa," amesema Samia.

Katika mkutano huo ambao mwenyekiti wake ni Makamba amesema kikao hicho kitatoka na azimio moja katika kukabiliana na majanga hayo.