Sunday, December 25, 2016

Mpango wa kushindanisha wakulima waiva

 

By Ben Patrick, Mwananchi bpatrick@mwananchi.co.tz

Geita. Halmashauri ya Mji wa Geita inatarajia kuwashindanisha wakulima wa pamba ikiwa ni moja ya hatua za kuinua uzalishaji.

Akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Bungw’angoko, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Modest Apolinary alisema shindano hilo litashirikisha kata zote zinazolima pamba.

Alisema lengo ni kuleta tija kwa wakulima ambao baadhi ya wameacha kulilima na kugeukia mazao mengine.

“Tutatazama kata ipi imepanda kwa kufuata kanuni za kilimo bora, kupalilia kwa wakati na matumizi sahihi ya dawa na mwisho ni uvunaji,” alisema Apolinary.

Miongoni mwa zawadi zitakazotolewa kwa kata zitakazoibuka washindi ni wakulima kusamehewa deni la mbegu.

“Pamoja na tija kwenye uzalishaji, vigezo vingine ni jinsi wakulima wanavyozingatia maelekezo ya maofisa ugani kuanzia kwenye kupanda, kupalilia, matumizi ya dawa, uvunaji na uhifadhi wa pamba,” alisema.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Mainila Bukelele alitamba kuwa wakulima wao wataibuka washindi na kuiomba Serikali kuwafikishia kwa wakati pembejeo za kilimo kulingana na mahitaji na msimu.

-->